MWENYEKITI wa iliyokuwa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amedokeza kuwa kwa tabia na mwenendo
wao, watawala wamemsaliti Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Jaji Warioba amekemea pia tabia
ya
watawala kumtumia Mwalimu Nyerere kama hirizi wanapotaka kupitisha mambo
yao, huku wakimsaliti kwa matendo yao.
Akizungumza katika kipindi cha
dakika 45 cha ITV juzi, Jaji Warioba aliwajibu viongozi wa serikali, wana CCM
na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaomshambulia kwamba amemsaliti Mwalimu
Nyerere.
Alisisitiza kuwa kamwe
hajamsaliti Baba wa Taifa Julius Nyerere kwa kuleta mapendekezo ya serikali
tatu, bali tume imetazama mapendekezo na hali halisi ya wakati tuliomo.
Badala yake Jaji Warioba amesema
kuhusu kumsaliti Mwalimu kuwa; Mwalimu Nyerere hakuwa na mawazo ya mgando, kwa
hiyo wasingemtegea kwamba wakati wote yale aliyokuwa nayo kama angekuwepo
angekuwa na hayo hayo.
“Mwalimu alikuwa anafuata wakati
ulivyo, lakini kubwa zaidi hao wanaosema hivyo ndio wamemsaliti Mwalimu…
Nilisema Mwalimu ametuachia muungano ambao Bunge la Muungano lilikuwa na
madaraka kamili, wameharibu… Mahakama ilikuwa na madaraka kamili wameharibu.
“Aliacha nchi moja, wamezigeuza
nchi mbili, wakati wa Mwalimu mizinga ilikuwa inapigwa kwa rais wa nchi, sasa
hivi wanapiga mizinga kwa marais. Wamevuruga muungano, hawaambiliki
wanakimbilia kumgeuza Nyerere kama hirizi,” alisema.
Jaji Warioba alifafanua kuwa
wakati wa Mwalimu mambo 22 ya muungano yaliyomo kwenye katiba, alipotoka kama
rais yalikuwa 21 na lile la 22 kuhusu vyama vya siasa lilikuja baadaye.
“Lakini hata Rais Kikwete
alipokwenda kwenye Bunge la Katiba alieleza kila moja ya mambo yale yaliingiaje
kwenye katiba na lini yaliingia. Yaliingia kikatiba, wao wameyaondoa kinyemela
bila kupitia katiba.
“Mwalimu alikuwa analinda katiba,
sasa wanasema mimi msaliti… Leo Mwalimu angetoka akaona haya aliyowatendea,
angesema mimi ndiye msaliti ama wao?” alihoji.
Alisema kuwa viongozi wamevuruga
muungano aliowaachia, lakini wanapoulizwa wanamtumia Nyerere kama
hirizi bila kutenda wasemacho kama alivyofanya yeye.
“Kwa kuwa wanazo microphone (vipaza
sauti) pale bungeni, wanaweza kusema hivyo, lakini je, kweli wanatenda kama
Mwalimu au wanasema tu?” alisema.
Kuhusu serikali tatu kuelea kama
wanavyodai CCM, kwamba haikopesheki na haina ardhi, Jaji Warioba alisema hoja
hiyo ni kuzungumza mambo ya upande mmoja wa Tanganyika, kwa sababu ndani ya
serikali mbili Zanzibar itaendelea kutohusishwa katika muungano.
Juu ya madai ya jeshi kupindua
serikali endapo mfumo wa serikali tatu utapita, alisema hii ni hatari sana kwa
wanasiasa kutumia mbinu za kushawishi umma kwa maslahi ya kisiasa ili waendelee
kubaki madarakani.
“Kwa hili ni kama unataka
kuchochea kwa kuwa unataka serikali mbili sasa watishe wananchi, msipokubali
serikali mbili jeshi litachukua madaraka. Kwa maana nyingine unaliambia jeshi
ni baya, litachukua madaraka. Kuna sababu gani ya kufika hapo?
“Unataka kuchochea jeshi liasi
kwa kisingizio kwamba hawalipwi mishahara, kwanini jeshi lisilipwe na sio
mawaziri au watumishi wengine?” alisema.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, Bunge
la Katiba lilianza kwa kusuasua kidogo kwa kuchukua muda mrefu kutengeneza
kanuni na kufarakana kidogo mwanzoni.
“Sisi tulipofanya kazi,
tulikwenda kuchukua maoni ya wananchi na wakati ule tulileta mapendekezo ambayo
tulidhani ni ya kuwaunganisha wananchi.
“Kwa hiyo tulichotegemea Bunge
nalo lingekwenda kwa hatua hiyo, lakini tangu mwanzo likaonekana kwamba
limejiunda katika makundi badala ya kujielekeza kwenye suala lenyewe kwa
kuangalia mawazo waliyoleta wananchi yanawekwaje ili tupate kitu cha
kuwaunganisha,” alisema.
Kuhusu kuchakachua maoni ya
wananchi na mabaraza, alisema kuwa katika rasimu ya kwanza walikusanya maoni ya
wananchi bila kufuata ni kundi gani wapate maoni.
Alisema kuwa rasimu hiyo
ilipotoka wananchi kwa asilimia kubwa waliona maoni yao yamo ila baadhi
yalihitaji kurekebishwa.
“Tulipokwenda kwa wananchi
hatukuwa na muundo, bali tulitaka watu waseme, ndiyo maana mawazo yote
waliyachukua na kuyatafsiri na tulipotoa rasimu ya kwanza tulitaka watu wapitie
kila ibara ili waone kama maoni yao yaliwekwa walivyotaka.
“Wananchi wale walikuwa na mambo
yao waliyotaka yawemo kwenye katiba, hivyo tuliwapelekea waangalie. Lakini
wakubwa hawa wakaenda na kuzunguka wakiwataka washughulikie suala la muungano
tu bila kujali kuna mengine. Kwa hiyo waliona hiyo ya madaraka tu wakataka kuifanya
hoja ya wananchi,” alisema.
Kuhusu ulazima wa serikali tatu,
alisema wakati wa kukabidhi rasimu ya kwanza alisema kuwa ili tuendelee na
muundo huu wa sasa wa serikali mbili, kunahitajika ukarabati mkubwa na kwa
tathmini ya tume iliona ni vigumu ndiyo maana wakapendekeza serikali tatu.
Alisema kuwa ameona tatizo kubwa
kwa wajumbe wa Bunge la Katiba wakizungumzia takwimu za tume yake wakidai
zimechakachuliwa, lakini ukweli ni kwamba zile takwimu ni za kweli.
“Hatukupeleka mapendekezo kwa
sababu watu wengi wamesema hivyo, bali tuliangalia hoja. Wanaohoji takwimu hizo
wapate majibu kwa Watanzania ambapo Zanzibar wanasema Tanganyika imevaa koti la
Mungano na Watanganyika wanasema Zanzibar imemega mamlaka kwa kujigeuza nchi
kamili,” alisema.
Mjumbe wa tume
Naye mjumbe wa tume hiyo ambaye
aliomba jina lake lisitajwe gazetini kwa madai kuwa wamechoshwa na matusi ya
wana-CCM wenzao, alisema kuwa walisimamia sheria na hadidu za rejea, lakini
akashangaa kuona wanaandamwa.
Kada huyo wa CCM alieleza
kuchoshwa na unafiki wa viongozi wakuu wa serikali zote mbili za Tanzania Bara
na Zanzibar akisema kuwa walipokutana na tume yao waliunga mkono serikali tatu,
lakini sasa wanajigeuza bungeni na majukwaani wakidai walilishwa maneno.
“Tuna taarifa nyingi kwenye tume
na ushahidi wa kutosha, maoni ya Rais wa Zanzibar, Ofisi ya Waziri Mkuu na
Baraza la Mawaziri yalikuwa ya serikali tatu ila nimeumia kuona tabia hii mbaya
ya kuwa na ndimi mbili,” alisema.
Mjumbe huyo pia alielezwa
kushangazwa na kitendo cha Bunge Maalumu kubadili kanuni zake ili kuruhusu
kuingiza sura mpya akisema ni kwenda kinyume na rasimu.
“Kuna baadhi ya wabunge
wanasikika wakisema kuwa mimi nimetumwa na wananchi wangu kuja kusema msimamo
wao ni serikali mbili. Je, walitumwa kwa mujibu wa sheria ipi? Sheria ya
Mabadiliko ya katiba inaruhusu wapi mbunge kwenda kukusanya maoni na kuyaleta
bungeni?” alihoji.
Alisema ni kama vile viongozi
hawajaona kuna tatizo baada ya wajumbe wa UKAWA kutoka nje, kwani CCM
wameendelea na majadiliano na kubadili kanuni, huku wakisema wanataka yafanyike
maridhiano na wenzao.
“Mwenzako akitoka hakuna tena
mjadala. Kama upo kwenye mgogoro wa ndoa, mwenzako ametoka wewe unayebaki
unasuluhishwa na nani?” alihoji.

Chapisha Maoni