SUKU moja baada ya vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kueleza kusudio lao la kufungua
kesi Mahakama Kuu kuhoji mamlaka ya Bunge Maalumu la Katiba, Mwenyekiti Kamati
ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, William Ngeleja, amewataka kurudi kwenye
meza ya majadiliano ili kupata muafaka.
Akizungumza na Tanzania Daima
jana katika viwanja vya ofisi ndogo za Bunge, Ngeleja alisema kuwa suala la
UKAWA kutoka nje si jambo jema na kuwataka warejee ili watunge katiba ya
wananchi.
Ngeleja ambaye pia ni Makamu
Mwenyekiti wa Kamati Na. 9 ya Bunge Maalumu la Katiba, alisema kuwa UKAWA
kuendelea kuwa nje ni kutowatendea haki wananchi ambao wana kiu ya mabadiliko
ya katiba yao.
Akijibu swali lililomtaka kueleza
hatua iliyochukuliwa na UKAWA ya kwenda mahakamani, Ngeleja alisema kuwa sheria
iko wazi na hawazuiwi ili wakapate ufafanuzi wa kisheria.
Akizungumzia utata wa kupatikana
theluthi mbili ya kura kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, Ngeleja alisema kuwa
Bunge Maalumu la Katiba lina mamlaka kamili na sheria namba 83 ipo wazi.
“Sheria inaeleza mamlaka ya Bunge
Maalumu la Katiba yaliyotajwa katika kifungu cha 25 cha sura hiyo ambayo
yanaruhusu mamlaka ya Bunge kujadili na kupitisha masharti ya katiba
yanayopendekeza mpito wa masharti mengine kama Bunge hilo litakavyoona.
“Kifungu namba 26 (1) kinalipa
Bunge Maalumu la Katiba uwezo wa kutunga kanuni kwa ajili ya kuendesha Bunge
hilo, kutokana na mamlaka kanuni zilitungwa na Bunge Maalumu la Katiba kusaidia
kuendesha mjadala wa katiba mpya,” alisema.
Alisema kuwa kutokana na mamlaka,
Bunge la Katiba lina uhalali wa kuweza kujadili, kurekebisha, kubadili na
kuondoa mapendekezo yoyote yaliyomo katika rasimu ya katiba.
Aliongeza kuwa uwepo au
kutokuwepo kwa UKAWA katika Bunge hilo linalotarajiwa kurejea Agosti mwaka huu,
hauthibitishi kupatikana kwa theluthi mbili.
Ngeleja alitamba kuwa kamati yake
ilifanikiwa kuongoza makubaliano yote katika kupata theluthi mbili bila kujali
tofauti za makundi.

Chapisha Maoni