WATU 18 wamefariki dunia,
wakiwemo polisi wanne na viongozi wote wa kijiji katika ajali mbaya iliyotokea
Kijiji cha Utaho, Kata ya Puma wilayani Ikungi, Mkoa wa Singida, ikilihusisha
basi lenye namba za usajili T 799 BET aina ya Nissan mali ya Kampuni ya Sumry.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Singida, Geofrey Kamwela, alisema kuwa ajali hiyo ilitokea wakati wananchi na
askari polisi wa doria walipokuwa wamekusanyika kando ya barabara hiyo,
wakijiandaa kuupakia mwili wa mwendesha baiskeli aliyegongwa na lori katika
eneo hilo na kufariki dunia.
Alisema kuwa askari hao walikuwa
wakifanya kazi hiyo wakiwa ndani ya gari lao lenye namba za usajili PT 1424
lililokuwa limeegeshwa kando ya barabara.
Kamanda alifafanua kuwa ghafla
basi hilo liliwagonga watembea kwa miguu na kusababisha vifo vya watu 15 papo
hapo huku wengine watatu wakifariki dunia wakati wakipatiwa matibabu.
Alisema kuwa dereva wa basi hilo,
Paul Njilo mkazi wa Dar es Salaam, alipokaribia eneo walipokuwa askari,
aliligonga gari lao na katika kukwepa aliwagonga wananchi pamoja na askari.
Kwa mujibu wa Kamanda Kamwela,
dereva huyo hakusimama bali aliendelea na safari kisha akalitelekeza basi hilo
eneo la Ikungi, zaidi ya kiliomita 25 kutoka eneo la tukio na kutokomea.
Aliwataja askari waliokufa kuwa
ni F.849 D/CPL Boniface Magubika wa CID Wilaya ya Singida, F.6837 Pc Jumanne
Mwakihaba wa FFU Singida, G.7993 Pc, Novatus Tarimo wa ofisi ya RCO na G.8948
Pc, Michael Mwakihaba wa FFU Singida.
Pia aliwataja wengine waliokufa
kuwa ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Utaho, Ramadhan Mjengi; Paul Hamis,
Mwenyekiti wa Kijiji cha Utaho; Ernet Salanga, Mwenyekiti Kitongoji cha Utaho;
Said Rajab, Usirika Itambu, Chima Mughenyi, Salim Juma, Abeid Ramadhan, Mwinyi
Hamis na Issa Hussein wote wakazi wa Kijiji cha Utaho.
Kamanda Kamwela alisema miili ya
marehemu wengine wanne bado haijatambuliwa na ndugu zao na huku taratibu za
kitabibu zikiendelea, na kwamba imehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa
Singida.
Alisema kuwa majeruhi wawili
wamelazwa katika hospitali hiyo ya mkoa na wengine sita katika hospitali ya
misheni ya Malkia wa Ulimwengu, Puma.
Miili ya askari polisi
inatarajiwa kusafirishwa kwenda mikoani wanakotoka wakati wowote mara taratibu
za kipolisi zikikamilika, ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na ndugu zao wa Rombo,
Pwani, Mbeya na Iringa.
Akizungumzia kuhusu ajali hiyo,
Kamanda Kamwela alisema awali saa 1:30 usiku ilitokea ajali ya mtembea kwa
miguu, Gerad Zefania aliyegongwa na lori na kufa papo hapo.
Alisema kuwa upelelezi zaidi wa
ajali hiyo unaendelea ili kujua chanzo halisi cha tukio pamoja na kumtafuta
dereva wa basi.
Katika hatua nyingine, watua
wanaosadikiwa kuwa majambazi wakiwa wa silaha, wamemuua kwa kumpiga risasi
askari polisi mkoani Tabora na kumjeruhi mwingine mmoja.
Tukio hilo lilitokea juzi saa
2:00 usiku katika Kijiji cha Usoke, Kata ya Usoke, Wilaya ya Urambo.
Taarifa ya kuuawa kwa askari huyo
ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Kamishina wa Operesheni na Mafunzo wa
Jeshi la Polisi, Paul Chagonja wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Chagonja alisema kuwa askari hao
walikuwa wakielekea katika eneo la tukio baada ya kupata taarifa ya kufanyika
ujambazi eneo la Usoke.
Alisema kuwa askari hao wakiwa
njiani walishambuliwa na majambazi hao wanaodaiwa kufanya tukio la uporaji wa
kutumia silaha kabla ya kumuua askari huyo na kumjeruhi mwingine.

Chapisha Maoni