RAIS wangu, koo langu limenikauka
kama gae! Usiku na mchana nimekulilia wewe Bwana. Machozi yangu yamegeuka kuwa
ndiyo chakula changu.
Kwanini unakaa mbali nyakati za
shida? Taifa lako linaangamia, masikini wa nchi hii wanafanyiwa dhihaka na
kusukumizwa kuzimu!
Waliopaswa kuwaongoza sasa
wanajisalimisha kwa jeshi! Wamewatengenezea waja wako mazingira ya kumwaga da
mu
kwa sababu tu ya ulevi wao wa madaraka!
Bunge Maalumu la Katiba lilikuwa
ni mzaha aghali na wa aibu kubwa nchi hii haijapata kushuhudia katika historia
yake. Umesema mwenyewe kuwa umekuwa ukifuatilia mchakato huo tangu
ulipolizindua, lakini yaliyoendelea baada ya hapo yamekusononesha na
kukusikitisha.
Bunge lilijaa kila aina ya
uchafu. Matusi, maneno ya hovyo hovyo na lugha chafu zilizokuwa zinatolewa na
baadhi ya wajumbe havikuacha tofauti yoyote na yale tunayoyaona kwa walevi
tunaokutana nao tunapokatisha kwenye vilabu vyao vya pombe za kienyeji!
Ulipokuja kukaririwa tena na
chombo cha habari kuwa ukiliangalia kwa undani linakufurahisha, unawapa wakati
mgumu sana waliotaka kukutenganisha na uchafu huu.
Si kawaida aibu kumfurahisha mtu
makini! Madhali sasa Bunge la Katiba limekoma, tumwombe Mwenyezi Mungu alilaze
mahali pema, na wajumbe wake wakapumzike kwa amani hadi ukomo wa utawala huu!
Rais wangu, wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi na wabunge wa Bunge la Jamhuri hawakuchaguliwa na wananchi kuwa
wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba. Na hawa ndio wamekuwa kiini cha fujo na
mambo ya aibu.
Hali hii ndiyo iliyosababisha
Bunge kuwa na hawa wengi na hawa wachache. Hili lilikuwa kosa kubwa. Hii ni
hila iliyofanywa bila watetezi wa wananchi kuigundua.
Kwakuwa mchakato huu uliuanzisha
wewe binafsi, ungefanikisha ungetuzwa kwa haki na wala si kwa vijisifa vya
kufedhehesha vitengenezwavyo na wanadamu.
Nawe ukishapita jina lako
lingeenziwa na vizazi vingi vijavyo. Huja hukutambua kuwa ulichoanzisha
kilikuwa sawa na safari ya majini. Kama hujui kuogelea, hata wimbi dogo tu
linakubeba.
Baba, katika hili nia yako njema
imebebwa na mawimbi. Matumaini ya Watanzania kupata katiba bora chini ya
uongozi wako umeyafifisha mwenyewe! Madhali sasa Bunge la Katiba limekoma,
tumwombe Mwenyezi Mungu alilaze mahali pema, na wajumbe wake wakapumzike kwa
amani hadi ukomo wa utawala huu!
Rais wangu, wananchi wamefarijika
kwa habari kuwa jumuiya na taasisi za Kiislamu Tanzania zimeungana na maaskofu
mbalimbali kuwataka wajumbe wa Bunge la Katiba kuheshimu rasimu ya katiba
iliyowasilishwa kwa
mujibu wa sheria na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
mujibu wa sheria na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Viongozi wa dini ambao bado
hawajachakachuliwa na wanasiasa bado wapo! Tuendelee kuwasikiliza. Wanaotutaka
tuwaombee walevi hawa badala ya kuwakanya waache ulevi wamechakachuliwa!
Tuwapuuze bila kujali vyeo vyao
katika dini wanazoziongoza! Walevi wanaombewa? Maoni ya wananchi kama
yalivyokusanywa na tume ni sauti ya Mungu mwenyewe, lazima yaheshimiwe na wote.
Wenye hila ya kutaka kuyapindisha
laana ya Mungu wetu na iwe juu ya kichwa chake na juu ya nyumba yake! Kama
Samuel Sitta alidhani Muadhama Polycarp Kardinali Pengo na Sheikh Mkuu Mufti
Shaban bin Simba ndio pekee wa kusikilizwa, alikuwa anajidanganya mwenyewe!
Muda wake wa kutumika hata ki-hila umekwisha.
Rais wangu, walioendelea na Bunge
baada ya wengine kususa walikuwa wahuni. Waliacha kujadili rasimu wakawa
wanajadili watu waliotoka.
Upunguani huu ulisababisha
wananchi kudhulumiwa kiasi kikubwa cha fedha, laki tatu kila siku! Wahuni wa
aina hii wanastahili kabisa kudharauliwa na kila mwenye mapenzi mema na nchi
hii! Wanaodhani wanaweza kufanikisha katiba mpya kwa hila, hawajui kuwa
kwakufanya hivyo, wanakupatiliza wewe baba uliyeanzisha mchakato mzima!
Wanataka wananchi wadhani
ulianzisha kitu ambacho ulikuwa hujui ukubwa wake. Kuiingiza nchi katika zahama
kubwa kama hii lazima uwajibike!
Wakati huo ukifika, baba hao
wasaka tonge hutamwona hata mmoja! Utakuwa peke yako! Ndipo maneno ya
mwanamwema Alto Makombwe wa Geita yatakapotimia.
Alisema: “Lakini kwa sababu wewe
unaandika ukweli siku itafika utaenziwa na kutuzwa!” Ndugu Rais, madhali sasa
Bunge la Katiba limekoma, tumwombe Mwenyezi Mungu alilaze mahali pema, na
wajumbe wake wakapumzike kwa amani mpaka ukomo wa utawala huu!
Kingunge mkana dini, mwana wa
aliyekuwa Katekista wa Kanisa Katoliki kule Kilwa Kipatimu enzi zile, marehemu Ngombale
Mwilu kaibuka kutoka katika kundi la waganga wa kienyeji na kusema kuwa Bunge
Maalumu la Katiba limekuwa ni mateso kwani lugha za matusi na kuzomea
viliwadhalilisha mbele ya wananchi!
Anachoshangaza Kingunge ni kutoa
kauli hiyo siku ya mwisho. Tangu mwanzo lugha hizo ndizo zilizokuwa zinatawala,
alikuwa wapi?
Pamoja na kupewa nafasi nyingi
hakukemea hali hiyo hata mara moja. Wala hakumkanya Mwenyekiti wa Bunge hilo
asiendelee kushabikia hali hiyo kizuzu kama wengine. Ameshuhudia Baba Warioba
na wenzake wakikashifiwa na kutukanwa tangu mwanzo hadi mwisho.
Leo ndiyo anasema waliomkashifu
Warioba ni wapuuzi waliokengeuka. Muda wake wa matumizi hata ki-hila
umekwisha!
umekwisha!
Rais wangu, zamani mvi zilikuwa
ni ishara ya busara! Kwa mvi zake na za Mwenyekiti wa Bunge na wengine wengi
waliokuwamo humo, wananchi hawakutegemea wafikishwe hapa walipofikishwa!
Wenye kutukana na wenye lugha za
hovyo hovyo wengi walikuwa ni vijana ambao walidhani matusi yangeweza kujazia
uwazi mkubwa uliomo ndani ya vichwa vyao.
Walipotoka waliotoka ndipo
ikajulikana walevi walikuwa ni akina nani.
Wakaonekana wakielea kama mafuta
yaeleavyo juu ya maji! Badala ya kujadili rasimu wakawa wanajadili serikali
tatu. Hawakujadili serikali mbili, lakini wenye upungufu mkubwa walikiri ujinga
wao hadharani kwa kumalizia kuwa: “Mimi ni muumini wa serikali mbili!
Waliowaomba waliotoka warudi kwa
kuwatukana waliwathibitishia wananchi ujinga wao bila kuacha shaka yoyote!
Sauti za wajinga zilisikika zikisema: “Wasuse wasisuse katiba lazima
itapatikana.” Mjinga zaidi yao akasema ataingia msituni!
Naye mwana wa shetani akamkumbuka
baba yake kwa kudhani kuwa waliosusa walikuwa ni baba zake wadogo, akawaita
shetani jina la baba yake.
Katiba ni maridhiano! Itakuwa ni
katiba ya aina gani hiyo itakayopatikana bila maridhiano? Upumbavu ni kilema,
ujinga una nafuu!
Kwa muda wote huo na pesa zote
hizo wamejadili sura mbili tu, nazo kipengele kimoja kimoja tu ambavyo hata
navyo havijaeleweka wameafikiana nini.
Hawa ndio viongozi wetu! Sijui ni
mikosi gani tulizaliwa nayo! Ndugu Rais, madhali sasa Bunge la Katiba limekoma
tumwombe Mwenyezi Mungu alilaze mahali pema, na wajumbe wake wakapumzike kwa
amani hadi ukomo wa utawala huu!
Rais wangu, mwanamwema Robbie
Natai akanitumia ujumbe akisema: “Mwalimu, hebu niulizie hawa watu waliopo
Dodoma maana Watanzania wengi tunawashangaa na zaidi ya yote tunapata machungu
moyoni.
Wajumbe hao wanaikataa rasimu
iliyowasilishwa na Baba Warioba, sasa wanajadili rasimu ipi?”
Naye Leonard kutoka Kigoma
akaniandikia: “Mwalimu, hawa watu hawana uchungu na sisi! Kwao katiba ni ile ya
ulinzi wa madaraka yao. Kama walikuwa na rasimu yao, ni kwanini wanateketeza
pesa zetu? Si waandike hayo wanayoyataka waondoke huko Dodoma? Wana bahati
wanawatawala watu wapole au niseme wajinga! Kwanini tusitoke wapenda nchi wote
tukawafurushe tuokoe fedha zetu? Mimi nafurahia mafundisho yako ya kila
Jumatano. Mungu akubariki sana.”
Rais wangu, Bunge unalosema
linakufurahisha limekoma, lakini haya ndiyo machungu lililowaachia wananchi.
Nani mwenye mapenzi mema na nchi hii atalitamani au kumtamani muasisi wake?
Pepo mchafu ameingia nchini
mwetu! Madhali sasa Bunge la Katiba limekoma, tumwombe Mwenyezi Mungu alilaze
mahali pema, na wajumbe wake wakapumzike kwa amani hadi ukomo wa utawala huu!
Upuuzi mwingine sasa basi!
Chapisha Maoni