Dar es Salaam. Ongezeko la
kasi ya ujangili nchini limedaiwa kusababishwa na vitendo vya rushwa, matumizi
mabaya ya madaraka na mfumo dhaifu wa usimamizi wa sheria katika Wizara ya
Maliasili na Utalii.
Kwa mujibu wa ripoti iliyopewa
jina la Urasimishaji wa Ujangili wa Kitaalamu
Afrika, tangu mwaka 2000 wizara
hiyo imejikuta katika kashfa za rushwa na kusababisha mawaziri na watendaji
wakuu kuvuliwa nyadhifa zao.
Katika ripoti hiyo, Taasisi ya
Kimarekani ya Utunzaji Wanyamapori ya Born Free USA kwa ushirikiano na Shirika
la Ripoti za Kichambuzi na Takwimu la C4ADS, imeeleza pia jinsi vikundi vya
waasi barani Afrika wanavyoendesha shughuli za ujangili.
Ripoti hiyo iliyozinduliwa mwezi
huu nchini Kenya, inaitaja Tanzania kama kitovu cha kusafirisha pembe za ndovu
katika ukanda wa Afrika Mashariki na Bandari ya Dar es Salaam imekuwa
ikishindana na ile ya Mombasa katika kutumia bandari kibiashara.
Kutoka mwaka 2008 mpaka 2013,
inaelezwa zaidi ya tani 20 za pembe za ndovu ama zilikamatwa zikisafirishwa
kuingia au kutolewa katika Jiji la Dar es Salaam, hii ni kwa mujibu wa taarifa
ya Taasisi ya C4ADS.
Ripoti hiyo inafafanua kuwa
uchunguzi wa vinasaba (DNA), katika tani 11 za pembe za ndovu zilizokamatwa
Taiwan, Japan na Hong Kong mwaka 2006, ilibainika kuwa pembe 1,500 zilitoka
Tanzania (Selous).
Uchunguzi huo ulibaini kuwa
vinasaba vya pembe hizo vilifanana, hivyo kujenga dhana kwamba baadhi ya watu
wamekuwa wakiwinda katika hifadhi hiyo mara kwa mara katika utaratibu maalumu
unaotambuliwa na Serikali.
“Kuna udhaifu mkubwa katika
usimamizi wa uwindaji halali na wawindaji wenye vibali hawasimamiwi ipasavyo
kufanya uwindaji kwa taratibu zilizowekwa kisheria. Hivyo hutumia nafasi hiyo
kufanya vitendo vya ujangili,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Serikali yakanusha
Hata hivyo, Mkurugenzi wa
Wanyamapori, Paul Sarakikya alikanusha madai hayo akisema siyo kweli kwamba
wawindaji halali huachwa bila usimamizi, bali wana mifumo ya kusimamia shughuli
hiyo.
“Sikubaliani na ripoti hiyo,
tumeshaongea sana juu ya suala hili, Rais alishalizungumzia na waziri pia.
Ufafanuzi ndio huo, hamna ukweli wowote katika ripoti hiyo,” alisisitiza
Sarakikya.
Salakikya alisema idadi ya tembo
nchini inazidi kuongezeka katika hifadhi tofauti na upungufu unaoelezwa katika
ripoti hiyo.
Mkurugenzi huyo alihoji kuwa kama
hakuna usimamizi madhubuti katika uwindaji halali, wamewezaje kusimamia
uwindaji miaka yote mpaka idadi ya tembo inaongezeka, baada ya upungufu
uliokuwepo miaka ya nyuma.
Wakati Sarakikya akisema tembo
wanaongezeka, ripoti hiyo inaeleza kuwa idadi ya tembo katika hifadhi za Selous
na Mikumi kwa mwaka 1976, ilikuwa ni 109,419 lakini kufikia mwaka 2009, idadi
hiyo ilishuka hadi kufikia tembo 38,975.
Nchi zilizoathirika zaidi na
ujangili barani Afrika, zinatajwa kuwa ni Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Cameroon, Msumbiji, Kenya, Zimbabwe na Tanzania
ambayo pia inatajwa kuwa kitovu cha usafirishaji wa pembe za ndovu.
Idadi ya tembo waliosalia
Na kwa utafiti uliofanywa na
Taasisi ya Frankfurt Zoological Society mwishoni mwa mwaka 2013, ripoti hiyo
inaeleza kuwa ni tembo 13,084 wanaokadiriwa kusalia katika hifadhi, sawa na
upungufu wa asilimia 66 katika kipindi cha miaka minne tangu 2009.
Hii imefafanuliwa kuwa zaidi ya
tembo 25,000 waliuawa katika Hifadhi ya Selous ndani ya miaka minne pekee. Pia,
ripoti hiyo inabainisha upungufu wa tembo katika hifadhi ya Ruaha-Rungwa kutoka
tembo 35,461 mpaka tembo 20,090 sawa na upungufu wa asilimia 36.5 kuanzia mwaka
1990 mpaka sasa.

Chapisha Maoni