Bila shaka kila mwananchi
anayeitakia mema nchi yetu amevutiwa na habari zilizochapishwa katika gazeti
hili jana kwamba vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa), vimeamua kushirikiana katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa kusimamisha
mgombea mmoja katika nafasi ya urais, ubunge na udiwani.
Viongozi wakuu wa vyama hivyo
tayari
wamekubaliana kuanza mchakato huo na wameandika mapendekezo na
kuyapeleka katika sekretarieti za vyama vyao kwa ajili ya kufanyiwa uchambuzi.
Sisi tunaona kitendo hicho cha
vyama vinavyounda Ukawa kuwa ni hatua muhimu ya kuongeza nguvu ili kuongeza
ushindani ambao ni muhimu katika mustakabali wa nchi yetu kisiasa na hivyo
kusaidia nyanja nyingine za kiuchumi na kijamii.
Tangu kuruhusiwa tena kwa siasa
huru karibu miaka 22 sasa, bado nchi haijashuhudia ushindani wa kweli unaoweza
kuwafanya watawala kuwajibika kwa wananchi kutokana na kuona hatari ya
kuondolewa madarakani na vyama pinzani.
Hii imetokana na vyama shindani
katika siasa kukumbwa na mifarakano ya kisiasa ambayo imekuwa ikiwagawa na
hivyo kuingia kwenye chaguzi vikiwa dhaifu na hivyo kushindwa vibaya na chama
tawala na matokeo yake yamekuwa ni wananchi wengi kukata tamaa na hivyo
kusababisha idadi ya wanaoshiriki kupiga kura kupungua mwaka hadi mwaka
kutokana na kutoona faida ya siasa za ushindani.
Pengine hiyo ndiyo sababu
iliyofanya wananchi wapendekeze kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwamba vyama
viruhusiwe kuunganisha nguvu wakati wa chaguzi kwa kuwa wameona bila ya nguvu
ya vyama shindani, watawala wawataendelea kuongoza kwa mazoea na matokeo yake
ni wananchi kuendelea na umaskini wao na kuona uhuru wa vyama vya kisiasa
hausaidii kuwa kuboresha maisha yao.
Si nia yetu kuona chama tawala
kikiondolewa madarakani na vyama shindani, lakini tunachotaka kuona na
ushindani wa dhati, makini na wa kweli ambao, kwa taifa lolote lile, ni afya
kwa ustawi wa wa taifa kwa kuwa huongeza uwajibikaji kwa watawala.
Hakuna ubishi kwamba upinzani
wenye nguvu huisukuma serikali ichape kazi na kuwatumikia wananchi kwa kutambua
kwamba ikiboronga itaondolewa madarakani na serikali kivuli ambayo ni vyama vya
upinzani.
Vyama legelege vya upinzani
huogopa kivuli cha serikali na kufifisha maendeleo na kuzima matumaini ya
wananchi wanaotaka kuona uwajibikaji serikalini, kwani huwa chachu ya
kuendeleza tawala za kiimla zisizothamini demokrasia na zisizowajibika kwa
wananchi.
Ndiyo maana tunawapongeza
viongozi wa Ukawa kwa kuona umuhimu wa kuunganisha nguvu na kuwa wamoja ili
kuweka ushindani wa kweli katika mazingira ya kisiasa tuliyomo.
Tunachoweza kuwashauri viongozi
wa Ukawa ni kuwa makini na kuondoa tofauti zinazowatenganisha. Ukawa isitarajie
kwamba kila kitu kitakuwa mteremko, kwani bado sheria kandamizi ambazo zimekuwa
zikikwaza shughuli za upinzani bado hazijafutwa.
Ni matarajio yetu kwamba serikali
na chama tawala kitachukulia hatua hiyo ya Ukawa kuwa changamoto ya kuongeza
ufanisi katika kuwatumikia wananchi na si kuanza kujenga chuki na kutafuta
mbinu za kuikwamisha.
Serikali haina budi kuhakikisha
kuwa vyama vyote vinapewa nafasi sawa ya ushindani na kujengewa mazingira ya
kukua ili kukifanya chama chochote kinachopewa madaraka kiwajibike kwa wananchi
na kuwaletea maendeleo.

Chapisha Maoni