Dar es Salaam. Siku moja
baada ya vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
kutangaza kusimamisha mgombea mmoja katika nafasi ya urais na ubunge majimboni,
CCM kimebeza hatua hiyo kikisema viongozi hao hawawezi kukaa zizi moja.
Akizungumza jana, Katibu wa
Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema
viongozi wa Ukawa ni genge la wasaka madaraka hivyo hawawezi kuungana kwa hilo.
Nnauye alisema viongozi wa vyama
vya upinzani waliungana kwa lengo la kutafuta Katiba bora, lakini wamebadilisha
ajenda na sasa wanazungumzia urais mwaka 2015.
“Hawa kumbe ni waongo, malengo
yao siyo Katiba, bali ni kutafuta madaraka, muungano wa kutafuta madaraka
hauwezi kufanikiwa kwa sababu viongozi wote wa Ukawa ni wapenda madaraka,”
alisema Nnauye.
Alisema wananchi watashuhudia
umoja huo ukisambaratika kwa sababu viongozi wa Ukawa hawawezi kuvumiliana na
kuachiana madaraka.
“Kuungana ni jambo zuri, lakini
sababu za kuungana zinapotajwa kuwa ni kumsimamisha mgombea mmoja wa urais
mwaka 2015, watasambaratika kabla ya muda huo kufika,” alisema.
Alisema Ukawa wamewadanganya
wananchi kwamba wanasimamia Katiba bora kumbe ajenda kuu ni kuongoza nchi.
Gazeti hili jana liliripoti kuwa
Ukawa pia wanataka kusimamisha mgombea mmoja wa ubunge katika kila jimbo la
uchaguzi.
Katika habari hiyo, Mwenyekiti wa
Chadema ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman
Mbowe, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Mwenyekiti wa NCCR
Mageuzi, James Mbatia walikiri kuwapo mpango huo.
Taarifa za kuwapo mpango,
zimekuja siku chache tangu kufichuliwa kwa mpango mwingine wa kuundwa upya kwa
Baraza la Mawaziri Kivuli ambalo litawajumuisha wabunge wa vyama vya upinzani
katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano wa bajeti
unaoanza Mei 6, mwaka huu.

Chapisha Maoni