Dar es Salaam. Vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vimeanza maandalizi ya
kushirikiana katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa kusimamisha mgombea mmoja katika
nafasi ya urais, gazeti hili limebaini.
Kadhalika, vyama hivyo ambavyo ni
Chadema, NCCR Mageuzi na CUF
vinakusudia kuwa na mgombea mmoja wa nafasi za
wabunge na madiwani, ikiwa ni hatua ya kuzikabili nguvu za chama tawala, CCM.
Habari zilizolifikia gazeti hili
zinasema tayari viongozi wakuu wa vyama hivyo wamekubaliana kuanza mchakato huo
na wameandika mapendekezo na kuyapeleka katika sekretarieti za vyama vyao kwa
ajili ya kufanyiwa uchambuzi.
Chanzo chetu kilidokeza kuwa
kamati ya wataalamu kutoka vyama hivyo tayari imeundwa ili kuandaa taratibu
zitakazotumika katika kufanikisha mkakati huo.
Wenyeviti wa vyama hivyo
walipoulizwa kwa nyakati tofauti kuhusu mpango huo hawakukubali moja kwa moja,
badala yake walisema ni mapema mno kuzungumzia suala hilo katika vyombo vya
habari.
Ukawa ni umoja ambao
uliviunganisha vyama vyenye malengo yanayofanana katika Bunge Maalumu la Katiba
na vimekuwa vikishinikiza kuzingatiwa kwa mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya
Katiba hususan muundo wa Muungano wenye serikali tatu, tofauti na serikali
mbili za sasa.
Umoja huo pia uliwaongoza wajumbe
wa Bunge Maalumu ambao ni wanachama wake kutoka nje kususia mchakato wa Katiba
Mpya kutokana na kile walichodai kuwa ni kutokuridhishwa na jinsi mambo
yanavyokwenda.
Taarifa za kuwapo kwa mpango wa
kushirikiana katika Uchaguzi Mkuu ujao, zimekuja siku chache tangu kufichuliwa
kwa mpango mwingine wa kuundwa upya kwa Baraza la Mawaziri kivuli ambalo
litawajumuisha wabunge wa vyama hivyo katika Bunge la Jamhuri wa Muungano wa
Tanzania.
Baraza la kivuli la sasa
linawajumuisha wabunge kutoka Chadema pekee, ambacho kinaunda Kambi Rasmi ya
Upinzani bungeni tangu kuanza kwa Bunge la 10, Novemba 2010.
Mwenyekiti wa Chadema ambaye pia
ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alisema atapanga upya
baraza lake katika siku za mwanzo za Bunge la Bajeti, linalotarajiwa kuanza Mei
6, mwaka huu mpango ambao umeungwa mkono na wenyeviti wa CUF na NCCR Mageuzi.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa
Ibrahim Lipumba alisema uamuzi huo ni hatua kubwa katika ushirikiano na kwamba
tayari alikwishawaarifu wabunge wa chama chake wawe tayari kushiriki katika
baraza hilo.
Mbowe alisema: “Hivi sasa suala
la sisi kuungana kwa maana ya kuwa na nguvu ya pamoja halikwepeki. Siasa ni
dynamic (zinabadilika), fikra za jana ni tofauti na fikra za leo kwa hiyo ni ukweli
usiopingika kwamba sisi wapinzani tunahitajiana kwa manufaa ya watu wetu na
nchi yetu.”
Hata hivyo, alisema ni mapema
kuzungumzia uwezekano wa ushirikiano wao katika vyombo vya habari na kwamba
wakati ukifika kila kitu kitawekwa wazi.
Kwa upande wake Profesa Lipumba
alisema: “Ningefurahi kama tungeweza kufikia kiwango hicho cha ushirikiano
maana kama unavyoona hatuwezi kusonga tusiposhikamana na kuwa wamoja, lakini
hilo siwezi kulizungumzia kwa sasa maana muda mwafaka bado.”
Aliongeza: “Ni kweli Katiba
imetuunganisha na huu ni mwanzo mzuri ambao unaweza kutoa mwanga kwamba huko
mbele tutakwenda vipi, tumeona kwamba Serikali haina nia njema kwenye suala
hili la Katiba, hivyo tukiendelea kutengana hatutaweza kuukabili udhalimu huu.”
Alipoulizwa wataweza kushirikiana
vipi na Chadema hali CUF wakiwa washirika wa CCM katika Serikali ya Umoja wa
Kitaifa (SUK) Zanzibar, Profesa Lipumba alisema mazingira yaliyowafanya kuingia
katika ubia huo yanafahamika kwani ulikuwa ni uamuzi wa Wazanzibari kupitia
kura ya maoni.
“Kuwamo katika SUK siyo tatizo
kwa sasa, siku zilizopita wenzetu walikuwa hawajatuelewa lakini sasa nadhani
tunakubaliana kwamba kuwamo kwenye Serikali huko Visiwani siyo kikwazo tena cha
kushirikiana na wenzetu,” alisema.
Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James
Mbatia alisema muungano wa vyama hivyo kupitia Ukawa limekuwa darasa kwa
viongozi wakuu wa vyama husika kutafakari walikotoka, walipo na wanakokwenda.
Hata hivyo, alisema ni mapema sana kuzungumzia suala la kuungana kwao
hadharani.
“Tunapata nafasi ya kutafakari na
kujifunza kwa kurejea tulikotoka kwa mfano hebu tuifikirie NCCR Mageuzi ya 1995
na ya sasa, CUF ya 2000 na 2005 na CUF ya leo na Chadema ya miaka iliyopita na
Chadema ya sasa, haya yote yanatupa fursa ya kutafakari kwa kina tunakotaka
kuupeleka upinzani katika nchi yetu,” alisema Mbatia na kuongeza:
“Kwa hiyo suala la kuungana siyo
la kujadili kwa sababu ndiyo mahitaji ya sasa, mjadala pengine ni kwamba
tunaungana vipi, katika maeneo gani na kwa madhumuni gani?”
Alisema katika siasa, chochote
kinaweza kutokea na kwamba mfano mzuri ni Kenya... “Hakuna aliyekuwa akiwaza
kwamba leo Rutto (William) angekuwa Makamu wa Kenyatta (Uhuru) kwenye
Serikali ya Kenya,” alisema.

Chapisha Maoni