Kilombero. Halmashauri ya
Wilaya ya Kilombero imeamua kufuta miliki ya mashamba yote makubwa
yasiyoendelezwa na taratibu mpya zinafanyika ili kuyamilikisha kwa wananchi.
Kati ya mashamba hayo, matatu ni
ya aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), marehemu Daudi
Balali na
aliyekuwa Katibu Mkuu wa Klabu ya Simba, Marehemu Priva Mtema yaliyoko katika
vijiji vya Lungungole na Merera ambayo wananchi wameshayavamia na kuendeleza
shughuli za kilimo.
Akizungumza katika kikao cha
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Kilombero juzi, Mwenyekiti wake, David
Ligazio alisema taratibu za kuomba hatimiliki za mashamba hayo zifutwe
zinaendelea.
Ligazio alisema wamiliki wa
mashamba hayo wameshapewa notisi na orodha yao imeshawasilishwa kwa Kamishna wa
Ardhi ili aridhie kufutwa kwa hati za mashamba hayo.
Alisema uamuzi wa kuyataifisha
umekuja baada ya halmashauri kubaini kuwa yamekuwa hayaendelezwi na hivyo
kusababisha maeneo hayo kuwa misitu wakati wananchi wanahitaji maeneo ya
kulima.
Alisema ukaguzi wa kumbukumbu
umeonyesha kuwa idadi kubwa ya wamiliki hao hawapo wilayani Kilombero na maeneo
hayo yanamilikiwa kwa hati za muda mrefu bila kufuata taratibu.
Alisema utaratibu unaofanyika
sasa ni kuwaagiza watendaji na wenyeviti wa vijiji, kuanisha ukubwa halisi wa
mashamba hayo ili kurahisisha kazi ya kuyagawa kwa wananchi katika siku zijazo.
Akizungumzia hatua hiyo, Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka alisema taarifa
hiyo haijafika ofisini kwake, lakini akabainisha kuwa kuna watu wengi
wanaomiliki ardhi kubwa mkoani Morogoro bila kuwa na hatimiliki wala kufuata
taratibu huku wakiwa wanawatisha wananchi.
Aliwataka wananchi hao
kujisimamia, waondoe unyonge na kuzingatia taratibu za ardhi, kwamba inatakiwa
kugawiwa kupitia mkutano mkuu wa kijiji, vinginevyo wana haki ya kujitwalia
maeneo hayo na kufanya maendeleo mengine.
“Kuna matukio unakuta mtu anakaa
na mwenyekiti wa kijiji na kujifungia, wanajadili wenyewe na kugawiana maeneo
ya kijiji bila kuwashirikisha wananchi, hawa wananchi wanatakiwa kukataa hali
hiyo,” alisema.
Maeneo yanayogawiwa
Mwenyekiti wa halmashauri
aliyataja maeneo mashamba yanayotakiwa kugawanywa kwa wananchi na ukubwa wake
katika mabano kuwa ni Lungongole (ekari 375) na Merea (ekari 373). Pia kuna
shamba lenye ukubwa wa hekta 887 linalomilikiwa na Balali, ekari 491
zinazomilikiwa na George Teni katika Kijiji cha Kisegese na ekari 500
zinazomilikiwa na Aloyce Lyenga katika Kijiji cha Idete.
Katika orodha hiyo pia kuna ekari
30,000 za Kampuni ya Merera Plantation Ltd katika Kijiji cha Merera.
Mashamba mengine ni ekari 102 za
Abdallah Sajiri zilizopo Kining’ina, ekari 295 za Peter Warwic zilizopo Lumemo,
ekari 484.9 za Sadru Meghji zilizopo Msolwa Ujamaa, ekari 120 za Ranifa EC
&DEV. Group zilizopo Kisegese na hekta 5,128 za Rubada zilizopo Ngalimila.
Ligazio alitaja mashamba mengine
kuwa ni ekari 2,390 za kampuni iliyokuwa ya usafirishaji mkoani Morogoro
zilizopo Mbingu, ekari 875 za Jerome Mwakifuna zilizopo Idete, ekari 656 za
Priva Mtemanyanja zilizopo Lungongole na ekari 1,500 za Ngwasi River Valley
Inv. zilizopo Mlimba.

Chapisha Maoni