WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera na Urataibu wa Bunge), William Lukuvi, amezidi kukaliwa kooni kwa
kutakiwa kujiuzulu kwa madai ya kutoa kauli za uchochezi kanisani.
Msimamo huo ambao ni wa pili
kutolewa dhidi ya waziri huyo, ulitolewa jana katika Msikiti wa Mtambani jijini
Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa kongamano la Jumuiya
na Taasisi za
Kiislamu zenye msimamo mkali.
Mbali ya kujadili kauli ya
Lukuvi, kongamano hilo pia lilijadili umuhimu wa kufanya maboresho kwenye
daftari la kudumu la wapiga kura, ambalo wanadai limekuwa likiwaacha nje baadhi
ya vijana wa Kislamu waliofikia umri wa kujiandikisha kupiga kura.
Kongamano hilo liliwakutanisha
watoa mada mashuhuri, wakiwemo maimamu wa misikiti mbalimbali kutoka
Tanzania Bara na Visiwani.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi
hao, Msemaji wa Taasisi hiyo, Sheikh Rajabu Katimba, alisema lengo la kukutana
na wanajumuiya hizo ni kufanya maazimio ya pamoja juu ya kauli za uchochezi
zilizotolewa na Lukuvi pamoja kujadili daftari la kudumu la wapiga kura.
“Bado tunaendelea na msimamo wetu
juu ya mchochezi huyo anayetaka kuvuruga amani, hatutaishia kwenye kongamano
hili, tutafanya nchi nzima na kutoa uelewa kwa Waislamu na Watanzania wapate
kujua madudu aliyosema Lukuvi,” alisema Katimba.
Alisema licha ya kusambaza nakala
kwa viongozi wakubwa wa nchi na Watanzania, wataendelea kulaani kauli ya Lukuvi
hadi Rais Kikwete atakapoamua kumwajibisha.
“Kauli za Lukuvi hazivumiliki
kwani ni hatari kwa taifa, kiongozi mkubwa kuongea vitu kama vile
haifai, tena badala ya kwenda bungeni kuomba radhi kwa Waislamu na
Watanzania, yeye kazidi kuonyesha uhodari wa kuchochea uvunjifu wa
amani,” alisema Katimba.
Aliongeza kuwa wamekuwa na utaratibu
wa kufanya makongamano mara kwa mara ili kutoa elimu zaidi kwa Waislamu,
pamoja na kujadili mchakato wa katiba na sio kwa Mkoa wa Dar es Salaam bali
watahakikisha wanazunguka nchi nzima kutoa elimu hiyo.
“Hatujasitisha makongamano,
tutaendelea kama kawaida mpaka tutakapopata muafaka juu ya kiongozi huyo,
la sivyo tutazidi kuongeza kasi ya kuwafikia Waislamu na Watanzania popote pale
walipo, na wakati huo tukifanya utaratibu wa kuchukua hatua za kisheria,”
alisema.
Kuhusu daftari la kudumu la
wapiga kura, Sheikh Katimba alisema liboreshwe kwani kuna vijana wa Kiislamu
waliotimiza umri wa miaka 18 mwaka 2014 na wengine mwaka 2013, lakini hawamo
kwenye orodha ya wapiga kura.
“Endapo vijana wetu waliotimiza
umri huo wa kupiga kura wasipoandikishwa kwenye daftari hilo,
hatutokubali na tutakuwa tayari kwa lolote lile mpaka kieleweke, pia
tutasimamia haki yao hadi ipatikane, kwani kuna vijana wetu wengi wanaachwa na
kukosa haki zao za msingi kumchagua kiongozi wanayemtaka,” alisema.
Aliilaumu serikali kwamba imekuwa
haizingatii kutenda haki kwa Waislamu katika masuala ya elimu.
“Tunaminywa haki zetu Waislamu,
Mahakama ya Kadhi imetupiliwa mbali, hata katika masuala ya kiuchumi bado
tunasumbuliwa, hasa kwenye Umoja wa Kiislamu (OIC), kwa mfumo huo hatutakubali
na tutadai haki zetu hadi kieleweke kupitia makongamano haya,” alisema Katimba.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya
Kiislamu na Mihadhara Zanzibar ya Uamsho, Abdallah Said Ally,
ambaye alikuwepo katika Msikiti wa Mtambani jana, alisisitiza kauli waliyoitoa
hivi karibuni ya kumtaka Lukuvi kuachia ngazi.
Kuhusu Muungano
Akizungumza katika kongamano
hilo, Sheikh Ali Baseleh, amesema kuwa mamadiliko ya katiba lazima yafanyike
kwa sababu ya katiba ya sasa ina kasoro kubwa katika muundo wa Muungano.
Sheikh Baseleh, alisema sio kweli
kuwa waliopendekeza na wanaounga mkono muundo wa serikali tatu, wanataka
kuvunja Muungano.
“Kama maoni ya wananchi kuhusu
serikali tatu yalikuwa hayatakiwi, kwanini zimetumika pesa nyingi kuunda tume
ili ishughulikie suala la katiba mpya?” alihoji.
Alisema wajumbe wa Bunge Maalumu
la Katiba, walipaswa kujadili maoni ya wananchi yaliyomo kwenye rasimu, lakini
waliyaacha na badala yake walikuwa wakipeana mipasho na kudhalilishana na hadi
lilipoahirishwa, hakuna jambo la maana lililokwishafanyika.
“Haya maoni ya wananchi yameletwa
kwa ajili ya kuboresha katiba kwa sababu ya sasa ina kasoro nyingi, leo Chama
Cha Mapinduzi (CCM) hawataki, wanataka kuleta maoni yao ya serikali mbili
ambayo hayamo kwenye rasimu,” alisema.

Chapisha Maoni