Msemaji wa Ikulu ya White House
ametaja uchaguzi wa Urais uliopangwa kufanywa nchini Syria kama "Mzaha wa
Demokrasia".
Jay Carney alisema matokeo ya
uchaguzi huo hayatatambuliwa nchini au nje.
Mpango wa kimataifa wa kisiasa
nchini humo unatarajia kuunda Serikali ya mpito ambayo itasimamia mambo hadi
Uchaguzi huru utakapofanywa.
Lakini Rais Bashar al-Assad
alisema hivi majuzi kuwa uhasama nchini humo umefikia kilele chake kwa sababu
ya hatua muhimu zilizofaulu kijeshi dhidi ya waasi. Wachanganuzi wa maswala ya
kisiasa wanasema kuwa angependa uchaguzi huo uthibitishe kuwa amethibiti
utawala nchini humo.
Tangazo la uchaguzi limefanywa
wakati ambapo habari zimepenyeza kuwa kemikali ya sumu imetumiwa katika
mashambulizi mapya nchini humo.
Marekani inasema kuna ishara kuwa
kemikali ya sumu, inayoshukiwa kuwa chlorine, ilitumiwa katika uwanja wa vita
mwezi huu na inachunguza iwapo Serikali ya Syria ilihusika.
Hadi kufikia sasa Syria imetajwa
kuondoa asilimia 65 ya silaha zake za kemikali kufuatia mapatano ya mwaka
uliopita yaliyoafikiwa baada ya shambulio lililowaua watu wengi ambalo mataifa
ya magharibi yalilaumu utawala wa Rais Assad

Chapisha Maoni