WAKATI mchakato wa kuandaliwa kwa
rasimu ya kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulipoanza na
kuwepo kwa rasimu ya pili iliyokabidhiwa kwa Rais Jakaya Kikwete ndipo
nilipojua kuwa kazi aliyopewa Jaji mstaafu Joseph Warioba haikuwa na tija
ndani ya Bunge Maalumu la Katiba.
Kumbe Jaji Warioba na timu yake
walipewa kazi ya kuongoza sherehe za Bunge Maalumu la Katiba na si kusherehekea
Jubilei ya Muungano ambayo kwa tafsiri ya haraka wenye sherehe wanaendelea
kufaidi matunda ya kuwemo ndani na mshereheshaji
akilipwa chake na kuondoka.
Nalazimika kuyaweka wazi mawazo
yangu hivi leo baada ya kushitushwa na kebehi, kashfa, mzaha na kuandamwa moja
kwa moja kunakofanywa na wanasiasa ambao hawana mlengo mahususi unaopaswa
kukubali na kuheshimu mawazo ya tume ya katiba iliyoundwa na rais mwenyewe.
Kibaya zaidi anayeandamwa sasa na
zaidi ya wajumbe wote walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kukusanya maoni ya
wananchi na kuandaa rasimu ya kwanza na ya pili, nyongo sasa imepasukia kwenye
moyo wa Jaji Warioba na si mwingine.
Jaji Warioba, mmoja wa waasisi
wakongwe na kada mashuhuri wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) sasa amegeuka kuwa jiwe
la pembeni lililokataliwa na waashi, ambaye haonekani tena kwa dhamira
yake na majukumu aliyopewa na rais ya kuiongoza tume ya katiba kuwa anautakia
mema Muungano.
Jambo la ajabu na la kusikitisha,
haieleweki ama Jaji Warioba alifanya kosa kwa kutokuwa na uelewa wa kutosha wa
kukubali kuwasilisha mapendekezo yaliyoandikwa kwenye rasimu ya pili ya katiba
kwa kutamka bayana kuwa kilichopendekezwa kwenye rasimu hiyo kilitokana na
maoni ya wananchi waliohojiwa kuwa wanahitaji muundo wa serikali tatu ndani ya
Muungano.
Kosa jingine ambalo pia
inawezekana, jaji huyo msomi alilifanya labda hakueleweka sawa sawa kama yale
aliyokuwa akiyasoma kabla ya Bunge Maalumu la Katiba halijazinduliwa na rais
yalikuwa maoni yake binafsi ndiyo maana amezalisha uhasama mkubwa kutoka kwa
Wana CCM chipukizi na wakongwe wenzake.
Ndiyo maana nathubutu kusema wazi
kuwa kitendo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji
Warioba kukubali au kushinikizwa kusoma rasimu ya pili ya katiba
bungeni kabla bunge hilo halijazinduliwa na rais hilo lilikuwa kosa kubwa la
kiufundi.
Inawezekana upotoshaji wa itifaki
na intelijensia za kisiasa kulichangia kwa kiasi kikubwa kumfanya jaji huyo aonekana
kama mwongoza sherehe za Bunge Maalumu la Katiba na haiba yake haikuonekana
wazi kuwa alipewa heshima kubwa ya kuongoza kazi ngumu ya kuandaa rasimu hiyo.
Matokeo yake sasa mwanasheria
huyo mkongwe, aliyewahi kuwa Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wa Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hapimwi tena kwa ukomavu wake wa kisiasa
ndani ya chama chake (CCM) na baadhi ya watendaji wa serikali alioweza
kuwafundisha kazi, sasa anaonekana kuwa ni msaliti.
Kuwa mapendekezo yaliyowasilishwa
na Jaji Warioba kabla ya bunge hilo kukamilisha kanuni zake na kuzinduliwa
rasmi na rais kwa baraka zote kumempotezea heshima zaidi jaji huyo mstaafu kwa
tabia na vitendo vinavyofanywa na vijana wadogo wa CCM kuwa kauli yake ya
kuwepo kwa muundo wa serikali tatu ni donda ndugu ndani ya muungano.
Wameamua kumnyoshea vidole kila
kukicha na kauli zinazotolewa na viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM)
kuwa chama chao hakikubaliani na mapendekezo ya serikali tatu yaliyowasilishwa
na Jaji Warioba, wakionyesha kung’ang’aniza kabisa muundo wa serikali mbili
zilizokuwepo tangu nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar zilipoungana mwaka
1964.
Inawezekana dhana ya woga na
upotoshaji inazidi kwa kasi kumuelemea Jaji Warioba na wengi wamesahau kuwa
wajumbe wa tume ya katiba hawakujiteua wenyewe nao waliteuliwa vilevile na Rais
Kikwete kwa kushirikiana na Rais wa Zanzibar, Dk. Mohamed Shein.
Kama walivyoteuliwa na marais hao
na kupewa baraka, ofisi na vitendea kazi vyote muhimu wasingeliweza kuandika
maoni yao kwa kushirikiana na sekretarieti iliyochaguliwa ili waweze kuchepusha
mawazo ya wananchi na kuandika kwa kina mtazamo na mapendekezo yao.
Wajumbe 201 wa Bunge
Maalumu la Katiba nao leo hii wanaweza bila shaka wakawa wameingia kwenye
mtego uliofanikisha kumnasa Jaji Warioba ili aonekane hadharani kuwa kazi
aliyotumwa kuifanya alishindwa na ndiyo maana alikuja na mapendekezo ya muundo
wa serikali tatu chini ya mwamvuli wa muungano.
Hayo yametokea lakini jambo la
aibu na fedheha hata kabla Jaji Warioba hajapandishwa kwenye mimbali kusoma
rasimu ya pili ya katiba, Bunge Maalumu la Katiba liligeuka kuwa uwanja wa
fujo, vurugu na malumbano kuhusu upitishaji wa kanuni, aliyekuwa Mwenyekiti wa
muda wa bunge hilo, Pandu Amir Kificho anajua kilichomkuta.
Kanuni ya 37 na 38 haikuweza
kupitishwa hadi alipokuja kuchaguliwa Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta,
vioja vya upigaji wa kura za ‘WAZI’ na ‘SIRI’ kulikochukua muda mrefu nako
kuliweza kuutafuna muda wa bunge hilo kwani idadi ya siku zilizopangwa zilizidi
kuyoyoma.
Hayo yote yametokea na
mashuhuda wa kila aina ya hoja kutolewa, kuzomeana, kuomba mwongozo
na kadhalika kumezidi kushamiri bungeni ilhali koti alilovaa Jaji Warioba
likiendelea kutoteshwa ndani ya bunge hilo, hawa wanataka serikali mbili na
hawa wanataka serikali tatu.
Jambo hili limegeuka kuwa kiini
macho kwa kuwa kamati za Bunge Maalumu la Katiba zilizoundwa nazo zinakumbwa na
jinamizi la theluthi mbili kukubaliana pale wanapohitaji kupitisha jambo, idadi
hiyo kwa upande wa Tanzania Bara na upande wa Tanzania Visiwani (nchi ya
Zanzibar).
Ndiyo maana naendelea kuiangalia
kazi kubwa iliyofanywa na Jaji Warioba na timu yake ilifanana na mshereheshaji
wa sherehe, mikutano au vikao (MC) ambaye hupatiwa kifuta jasho chake
anapomaliza kazi na wenye mahitaji nao wanaendelea na kazi yao ya kuvunja
kanuni.
Kama hayo yametokea na hali
inazidi kuwa tete ndani ya Bunge Maalumu la Katiba sioni kama ilikuwepo
haja ya kuundwa kwa Tume ya Katiba iliyopewa dhamana kubwa ya
kuongozwa na jopo la wasomi, pia kuundwa kwa Bunge Maalumu la Katiba
kunazidi kuwaongezea wananchi simanzi kwa kuwa pesa za walipa kodi zote
zinateketea ndani ya malumbano ya katiba mpya.
Jambo zito la kujiuliza iweje na
nchi inashindwa kufikia kwenye malumbano ya staha na busara kama kile
kilichojadiliwa na wananchi kikaonekana kinyume na fikra za watu wachache tu
kwa sababu Watanzania wapatao 629 wamejaliwa kuwa na sauti za malaika na
wengine zaidi ya milioni 45 wanaganga njaa uswahilini.
Basi niseme, kwa kuwa Jaji
Warioba amevalishwa gunia la chawa, kwa kusoma rasimu ya pili ya katiba
alipowasilisha mapendekezo yaliyoweka wazi na tume yake kuwa hayo ndiyo
maoni ya wananchi mshahara wake umebaki hobelahobela, kusimangwa, kupigwa
vita, kutolewa kauli zisizokuwa na staha na pengine anastahili hivi sasa
kunyang’anywa kadi ya CCM kwa kuwa hakubaliki na msimamo wa chama chake
haumuungi mkono, pole Jaji Warioba.
Inawezekana kabisa kuwa hayo yote
yanayoendelea kutokea hayakuwa matarajio ya Watanzania wengi kumuona Jaji
Warioba akisulubiwa bila kosa kila kona, naamini hata Yesu Kristo au Nabii Issa
alikutwa na kadhia zaidi ya hiyo wala asisononeke moyoni mwake bali awasamehe
waliomteua na kumuamini.

Chapisha Maoni