INGAWA ukweli wa haya nitakayoyaeleza ni PIGO jingine kwa
CHADEMA, naomba nitumie neno FUNZO, labda viongozi wake watanielewa vizuri. ‘Funzo’
ni jambo au kitendo kinachomrekebisha mtu tabia.
Funzo la kwanza lilikuwa uchaguzi wa madiwani ambapo CCM
kilizoa viti 24 na ‘kuwaachia’ CHADEMA viti vitatu tu.
Funzo la tatu ni uchaguzi wa mbunge wa jimbo la Chalinze
ambalo pia lilikuwa wazi baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wake, marehemu Said
Bwanamdogo. Aliyesimamishwa na CCM kugombea kiti hicho ni mwana wa Rais Jakaya
Kikwete, aitwaye Ridhiwani. CHADEMA kilimsimamisha Mathayo Torongei
aliyeangushwa kwa fedheha.
Wakati Ridhiwani akipata kura 20,828 sawa na asilimia 86.61,
alimwacha kwa mbali Mathayo Torongei aliyepata kura 2,544 yaani asilimia 10.6.
Mgombea Fabian Skauki wa CUF alipata kura 476, sawa na asilimia 1.98. Mgombea
Ramadhani Mgaya wa AFP alipata kura 186 sawa na asilimia 0.59, huku Hussein
Ramadhani wa NRA akiambulia kura 60, yaani asilimia 0.25.
Jimbo la Chalinze limekuwa chini ya himaya ya CCM tangu
lilipoanzishwa mwaka 1995. Mbunge wake wa kwanza alikuwa Jakaya Mrisho Kikwete
ambaye sasa ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayekaribia kumaliza
kipindi chake cha pili. Alifuatiwa na Ramadhani Maneno kisha Bwanamdogo
aliyefariki dunia kabla ya kumaliza kipindi chake na sasa ni Ridhiwani Jakaya
Mrisho Kikwete. Kama baba, mwana naye yu mumo humo.
Msimamizi wa uchaguzi huo, Samwel Sarianga, alisema
waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 92,000 lakini waliojitokeza kupiga kura
walikuwa 24,422. Hii ina maana wapiga kura 67,578 waliojiandikisha
hawakujitokeza kufanya zoezi hilo!
Soma walivyosema baadhi ya wananchi waliohojiwa baada ya
uchaguzi wa Chalinze: “Tutaendelea kushiriki mikutano ya kampeni za vyama
vitakavyokuwa vinatupatia chochote lakini hatutapiga kura kwani wote
tuliowachagua katika jimbo letu hawajatuletea maendeleo!”
Bado viongozi wa CHADEMA hawajapata funzo kwa matokeo hayo?
Hawajiulizi ni kwa nini idadi ya wapiga kura hupungua kila uchaguzi?
Hawajiulizi ni kwa nini wapinzani (wakiongozwa na CHADEMA) hupata kura kiduchu
vijijini na baadhi ya maeneo kutopata hata kura moja?
Mbele ya safari kuna uchaguzi wa wenyeviti wa serikali za
mitaa baadaye mwaka huu (kama hautaahirishwa) na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika
mwezi Oktoba mwaka 2015. Wamejipanga vipi kushinda? Au ni yale yale ya
kutosheka na wingi wa watu kwenye mikutano yao mijini huku wakiwa hawatambuliki
vijijini? Si wote wanaohudhuria mikutano yao wamejiandikisha kupiga kura wala hawajui
haki yao ya kufanya hivyo.
Mara kadhaa huko nyuma niliwaasa viongozi wa CHADEMA
waangalie walikojikwaa badala ya kuangalia walikoangukia. Mtu mjinga huishia
kujifunza kutokana na shida au taabu kwa sababu ya kupuuza ushauri. Hutumiwa
kumwelezea mtu aliyepuuza ushauri aliopewa kisha akaishia kutumbukia katika
matatizo mengi. Ni ufafanuzi wa methali ya “Fumbo la mjinga taabu.”
Viongozi wa CHADEMA wahamie vijijini kwa muda badala ya
kukurupukia operesheni ya M4C ya mpito. Wapige kambi vijijini kuwapa wanavijiji
elimu ya uraia, maana, umuhimu, faida za kujiandikisha na kupiga kura.
Wawaeleze na kuwafafanulia maana ya upinzani ili kuwaondolea hofu kuwa ni watu
wanaotaka kuleta machafuko nchini kama wanavyozugwa na CCM.
Tena kwa heshima na taadhima naomba pia niwakumbushe
methali isemayo: “Mtu haoni aibu yake huiona ya mwenziwe.” Kwa kawaida binadamu
hawazioni kasoro zao ila huziona za wenzao. Huweza kutumiwa kwa mtu mwenye
tabia ya kuwalaumu wenzake kutokana na aibu zao lakini hazioni zake mwenyewe.
Viongozi wa CHADEMA ndio waliokifanya CCM kitambue makosa
yake kwani kimekuwa kikificha madhambi mengi ya serikali yake. Hili ndilo
linalomzindua Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana, kukiri kuwa chama chake
kitakuwa na wakati mgumu katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 kujibu maswali
ya Watanzania kuhusu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010. Katika
miaka ya hivi karibuni haikuwa rahisi kiongozi mkuu wa CCM kuikosoa serikali.
Maneno kama haya ambayo zamani yalikanushwa kwa nguvu na
CCM, ndiyo yanayowapumbaza viongozi wa CHADEMA. Katika vita waweza kuwa na
silaha nzito za kisasa kuliko mpinzani wako lakini kama huna utaalamu na mbinu
ni bure.
CCM kina utaalamu na mbinu na ni wepesi wa kugeuza kibao
dakika za ‘lala salama.’ CHADEMA bado hakijapata utaalamu na mbinu kama hizo!
CCM kinajivunia mfumo wake wa uongozi unaowashirikisha
wajumbe wa nyumba kumi, mashina, matawi, kata, wilaya, mikoa mpaka makao makuu.
Kote huko makada wake hufanya mikutano kujadili mambo
mbalimbali yanayohusu chama chao kuendelea kushika hatamu. Utokeapo uchaguzi
wowote, makada hao hupita nyumba kwa nyumba usiku kuwahamasisha wananchi
wawapigie kura wagombea wao.
Huko ndiko wanakowasihi wananchi ‘kutosikiliza na kubeza
kelele na porojo za wapinzani, hususan CHADEMA.
Je, CHADEMA kina utaratibu kama huo huko vijijini? Au ni
mpaka wakati wa uchaguzi ndipo kinapoonekana kwa mbwembwe nyingi na matumizi ya
helikopta? Tuchukue mfano wa Dar es Salaam hususan Jimbo la Segerea. Uongozi wa
juu unajua kinachoendelea miongoni mwa viongozi wa jimbo hilo?
Uongozi wa Jimbo la Segerea umegawanyika makundi mawili.
Moja ni lile la viongozi wanaokusudia kugombea udiwani na ubunge wa jimbo
hilo kwa hali yoyote iwayo. Jingine linataka kukiimarisha chama kuanzia chini
lakini linapigwa vita na hao wanaoutaka udiwani na ubunge kwa udi na uvumba.
Viongozi wa misingi na matawi wenye msimamo hawaalikwi
kwenye mikutano ya jimbo wala viongozi wa jimbo hawatembelei misingi na matawi
na hawajui yaliko! Uozo huu unajulikana makao makuu ya chama?
CHADEMA kitajengwa vipi kwa mtindo huu? Kama viongozi wa
Segerea hawajui yaliko baadhi ya misingi na matawi chama kitakuwa na uhai?
Kama misingi na matawi yanabaguliwa kwa sababu viongozi wake
ni wakweli wasiopenda unafiki, CHADEMA kisitegemee kulitwaa Jimbo la Segerea
kirahisi kama inavyodhaniwa.
Viongozi wakuu wa CHADEMA wafanye hima kutembelea misingi na
matawi ili waone jinsi uhai wa chama wa Jimbo la Segerea unavyopelekwa arijojo.
Hili ni eneo moja tu mkoani Dar es Salaam bila kutaja maeneo mengine nchi
nzima. Kama viongozi wa CHADEMA hawatazinduka sasa, nadhani hata viti
walivyovitwaa kwenye uchaguzi wa mwaka 2010 watavipoteza.
Hali ikiwa hivyo viongozi wakuu watawaambia nini wananchi
waliokuwa wakiimbishwa “people’s” nao kujibu “Power!”?
Viongozi wakuu wa CHADEMA wajiulize ni kwa nini hushindwa
vijijini. Ndiko kunakokinufaisha CCM kwani kimeeneza mizizi yake
huko.
Nimeeleza mwanzoni kuwa CCM ni fundi wa utaalamu na mbinu.
Je, viongozi wakuu wa CHADEMA wana uhakika wa usafi wa nyumba yao? Wote
wanakipenda CHADEMA kwa dhati? Hakuna mashushushu wa CCM wanaokidhoofisha bila
wenyewe kujua?
Majuzi nilivutiwa na kipindi cha HOTMIX kinachorushwa na
runinga ya EATV wakati mkazi anayeishi mpakani mwa Tanzania na Malawi
alipouliza: “Serikali iliunda tume ya kupata maoni ya wananchi na ilitembea
nchi nzima kwa ajili hiyo ikitumia fedha za wananchi.
Sasa kwa nini serikali hiyo hiyo inaacha maoni ya wananchi
na kukazania ya kwake? Kulikuwa na sababu gani za kuunda tume kumbe serikali
ilikuwa tayari ina msimamo wake?”

Chapisha Maoni