LICHA ya Mwenyekiti wa Bunge
Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, kuruhusu uvunjwaji wa kanuni ili kuruhusu
wenyeviti wa Kamati za Bunge kufafanua baadhi ya mambo wakati wa uwasilishaji
wa taarifa zao, haikusaidia kupunguza mashambulizi ya wapinzani.
Kanuni ya 33 ya Bunge Maalumu
kifungu cha (4) na (5) vinaweka bayana kwamba baada ya mwenyekiti wa kamati
kuwasilisha taarifa ya kamati inayohusika, atamwita mmoja wa wajumbe wa kamati
aliyeteuliwa na wajumbe walioandaa maoni ya wachache kutoa ufafanuzi wa maoni
yao kwa muda usiozidi dakika 30.
Sitta, jana aliamua kuvunja kanuni hiyo kuwabeba wajumbe wa CCM waliokuwa wakilaumu wapinzani kupewa fursa kubwa ya kushambulia walio wengi huku mwenyekiti wa walio wengi akibanwa asifafanue jambo.
Sitta alisema ruksa kwa
mwenyekiti wa kamati kutoa ufafanuzi wa taarifa ya walio wengi badala ya kusoma
kama kasuku.
Hata hivyo mbeleko hiyo ya Sitta
ilishindwa kutumiwa kikamilifu na wenyeviti wa kamati namba tatu na namba nne
waliojikita zaidi kwenye ufafanuzi wa taarifa za kamati huku wakilenga kuminya
muda wa kuwasilisha taarifa ya watu wachache.
Mwenyekiti wa Kamati namba tatu,
Dk. Francis Michael, alitumia mwanya huo kutoa ufafanuzi wa mambo ambayo
hayakuwepo kwenye vitabu vya taarifa ya kamati yake vilivyogawiwa kwa wajumbe.
Kitendo hicho kilifanywa juzi na
Mwenyekiti wa Kamati namba moja, Ummy Mwalimu, wakati akiwasilisha taarifa ya
kamati yake.
Hatua ya Dk. Michael, kujikita
zaidi kutoa ufafanuzi badala ya kusoma taarifa ya kamati yake kilisababisha
wajumbe wachache kupiga kelele na kumzomea.
Wajumbe wachache walidai kuwa Dk.
Michael, alikuwa akifanya hivyo ili kuminya muda wao kwa lengo la kuzuia maoni
yao yasipate nafasi kama inavyotakiwa.
Dk. Michael, alitoa kioja baada
ya kugoma kusoma maoni ya walio wachache kwa madai amechoka.
Kauli hiyo ilichafua hali ya hewa
ndani ya Bunge na kuwafanya wajumbe wachache kusimama, kuzomea na kuimba; ‘CCM…
CCM…. CCM….’
Mwenyekiti wa Bunge, Sitta,
alimlazimisha Dk. Michael kusoma taarifa ya wajumbe walio wachache lakini
katika mshangao alisoma vichwa vya habari vya taarifa hizo huku akidai
watafafanua wenyewe.
Kitendo hicho kilimfanya Sitta
kuwakemea wajumbe waache kuzivuruga kanuni walizozitunga huku akimlazimisha
mwenyekiti huyo kusoma taarifa yote kama ilivyoandaliwa.
Dk. Michael, alikaidi agizo la
Sitta, hali iliyowafanya wajumbe wachache kuinuka kwenye vitu huku wakimzomea
na kumtaka aondoke kwenye eneo la kutolea hotuba.
Wachache hao walibainisha kuwa
mwenyekiti huyo alishasema tangu awali hatakuwa tayari kuisoma taarifa yao.
Mvutano huo ulihitimishwa baada
ya kuchaguliwa kwa mjumbe mmoja wa walio wachache, Mchungaji Peter
Msigwa, kusoma taarifa hiyo na kutoa ufafanuzi.
Katika ufafanuzi
wake, Msigwa alisema jina la Tanzania halina uhalali kwa sababu halipo
kwenye Sheria ya Muungano ya mwaka 1964.
Alisema katika sheria hiyo nchi
iliyoungana inayotajwa ni Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Jamhuri ya
Zanzibar.
“Hati ya Muungano haipo ndiyo
maana haitolewi, jambo hilo limezidisha utata wa uhalali wa Muungano,” alisema.
“Tunataka kusogea mbele lakini
hakuna taarifa sahihi kuhusu Muungano, watu wanafichwa mambo kuhusu
Muungano ambao sasa umekuwa kama fumbo la imani huku kero za Muungano
zikiendelea kuchipuka kama uyoga, hatuwezi kwenda huko bila kutatua matatizo
yetu,” alisema.
Alibainisha kuwa kitendo cha
Zanzibar kutunga katiba yao inayokinzana na ile ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kimevunja Muungano na kimeongeza kero zake.

Chapisha Maoni