Home » » Azam FC, Mbeya City zimetia fora Ligi Kuu

Azam FC, Mbeya City zimetia fora Ligi Kuu

Written By Unknown on Jumatatu, 21 Aprili 2014 | 02:27

KAMPENI ya miamba 14 kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara iliyoanza Agosti 24, mwaka jana, imefikia tamati mwishoni mwa wiki.
Ligi hiyo imehitimishwa kwa rekodi ya aina yake iliyowekwa na Azam FC, ambayo sio tu imetwaa ubingwa kwa mara ya kwanza, pia haikupoteza mechi hata moja.
Katika mechi zake 26 ilizocheza, imefanikiwa kushinda 18 na kutoka sare nane, hivyo kukusanya pointi 62.
Ni mafanikio makubwa ya kwanza kwa Azam iliyoanzishwa miaka saba iliyopita – Juni 24, mwaka 2007.
Kabla ya kutwaa ubingwa Aprili 19, Azam wakicheza ligi hiyo kwa mara ya kwanza msimu wa 2008/9, walimaliza nafasi ya nane kabla ya kumaliza nafasi ya tatu 2009/2010 kama ilivyokuwa msimu wa 2010/11.
Walimaliza nafasi ya pili msimu wa 2011/12, hivyo kupata nafasi ya kucheza michuano ya kimataifa kwa mara ya kwanza katika historia yao.
Wakicheza Kombe la Shirikisho (michuano ya pili kwa ukubwa katika ngazi ya klabu barani Afrika), walipambana hadi raundi
ya pili ambapo walitolewa na FAR Rabat ya Morocco.
Azam ikitoka kuwang’oa El Nasri ya Sudan Kusini na Young Barrack Controllers ya Liberia katika raundi ya awali na ya kwanza, walitolewa na FAR Rabat baada ya kufungwa jumla ya mabao 2-1.
Licha ya kung’oka, wachezaji wa Azam inayomilikiwa na mfanyabishara maarufu wa jijini Dar es Salaam, Said Salim Bakhresa, walizidi kuimarika dhidi ya mechi za kimataifa, hivyo kuzidi kuwa tishio dimbani.
Msimu wa 2012/13, Azam walifanikiwa kumaliza nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu, nyuma ya Yanga, hivyo kupata tena tiketi ya Kombe la Shirikisho.
Pamoja na timu hiyo kuishia raundi ya awali waking’olewa na Feroviarial da Beira ya Msumbiji, ilizidi kujifunza mengi zaidi juu ya ushiriki wake katika mechi za kimataifa.
Baada ya kutolewa Kombe la Shirikisho, wakahamishia nguvu zao zote katika kupigania ubingwa wa Ligi Kuu.
Akili za wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa klabu hiyo zikajikita katika kuipigania timu kubeba ubingwa huo kwa mara ya kwanza baada ya kuishia nafasi ya pili mara mbili mfululizo, na wakafanikiwa kutimiza ndoto hiyo wakisaliwa na mechi moja mkononi.
Japo walikabidhiwa ubingwa rasmi Jumamosi ya Aprili 19, Azam walishatwaa taji hilo tangu Aprili 13, walipowafunga Mbeya City kwa mabao 2-1, hivyo kufikisha pointi 59, ambazo zisingefikiwa na timu nyingine.
Azam ilimaliza ligi hiyo Jumamosi kwa rekodi ya kutofungwa, baada ya kuwafunga maafande wa JKT Ruvu bao 1-0 katika Uwanja wa Azam Complex, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na kufikisha pointi 62.
Azam pia imekuwa timu pekee iliyoweza kutoka na ushindi Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine dhidi ya Mbeya City baada ya kushinda 2-1 zilipokutana Aprili 13.
Wakati Azam wakibeba ubingwa, Yanga waliokuwa mabingwa watetezi, wakiwa na rekodi ya kubeba taji hilo mara 24, wamemaliza nafasi ya pili baada ya kufikisha pointi 56, wakishinda mechi 16, sare nane na kufungwa mara mbili.
Nafasi ya tatu imekwenda kwa timu ngeni ya Mbeya City iliyocheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu huu, ambayo imemaliza na pointi 49.
Mbeya City chini ya kocha wake Juma Mwambusi, licha ya ugeni wake, imeweza kushinda mechi 13, sare 10 na kufungwa tatu.
Nafasi ya nne imetwaliwa na wakongwe Simba ambao kwa mara ya pili mfululizo, wamekosa tiketi ya michuano ya kimataifa baada ya kushindwa kumaliza ligi katika nafasi mbili za juu.
Hata hivyo, katika uhalisia wa mambo unaweza kusema timu zilizotia fora katika msimu huu, ni Azam iliyobeba ubingwa kwa mara ya kwanza katika historia yao na Mbeya City waliomaliza nafasi ya tatu licha ya ugeni wao katika ligi hiyo.
Azam, imekuwa timu ya kwanza nje ya Simba na Yanga kujitwisha ubingwa wa Ligi Kuu tangu mwaka 2000, pale Mtibwa Sugar ilipofanya kweli, ikipeleka taji Turiani, Morogoro baada ya kuwa kinara pia mwaka 1999.
Kwa ujumla, Azam inakuwa timu ya saba nje ya wakongwe Yanga na Simba kutwaa taji la Ligi Kuu, baada ya Cosmo ya Dar es Salaam (1967), Mseto ya Morogoro (1975), Pan Africans ya Dar es Salaam (1982), Tukuyu Stars ya Mbeya (1986), Coastal Union ya Tanga (1988) na Mtibwa Sugar (1999 na 2000).
Matunda ya juhudi
Aprili 19 ya mwaka 2014, itabaki kuwa ya kipekee kwa wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa timu hiyo ambao walishuhudia matunda ya juhudi za uwekezaji wao kwa timu hiyo tangu kuanzishwa kwake.
Siku hiyo, wakurugenzi wake Abubakar, Omar na Yussuf Bakhresa wakiwa jukwaa Kuu na Rais wa TFF, Jamal Malinzi, walionekana wakiwa kwenye furaha ya aina yake ukiwa mwanzo mwingine mpya wa kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza.
Baada ya filimbi ya mwisho ya mechi yao dhidi ya JKT Ruvu, kilichofuata ni shangwe na nderemo kwa wachezaji, makocha, viongozi na mashabiki kujimwaya kufurahia mafanikio hayo.
Malinzi alimkabidhi Kombe la ubingwa nahodha John Bocco baada ya mechi hiyo pamoja na cheti maalumu kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), ambacho kinatolewa kwa mara ya kwanza mwaka huu, Azam ikiwa timu ya kwanza kukipata.
Wachezaji walivalishwa medali na baada ya hapo sherehe za ubingwa zilichukua nafasi yake Uwanja wa Azam Complex.
Kwa kadiri itakavyokuwa, Azam wanapaswa kupongezwa kwa kuonyesha soka safi katika msimu mzima, hivyo kumaliza ligi bila kupoteza mechi yakiwa ni matokeo ya kazi kubwa iliyofanywa na wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa timu hiyo.
Mbeya City nayo inabaki kuwa mfano wa kuigwa na timu nyingine ngeni katika ligi hiyo msimu ujao, yaani Stand United, Polisi Morogoro na Ndanda FC, ambazo zinapaswa kuwa washindani, si washiriki.
Naamini kama timu hizi ngeni zilizochukua nafasi ya Ashanti United, Rhino Rangers na JKT Oljoro, zitakuja na makali kama ya Mbeya City, kutaongeza ushindani na utamu katika Ligi Kuu.                 
Kitisho Simba, Yanga
Japo rekodi zinaonyesha kuwa Simba na Yanga ndizo zimekuwa zikipokezana ubingwa, lakini ni wazi ujio wa Azam umeanza
kuleta ufa na matatizo kwa wakongwe hao.
Mfano hai ni namna Azam ilivyong’ang’ania nafasi ya pili katika misimu miwili mfululizo huku Simba na Yanga zikipishana katika nafasi ya kwanza na tatu.
Msimu wa 2011/12, Simba ilimaliza ligi ikiwa bingwa huku Azam ikiwa ya pili nafasi ambayo waliitetea tena msimu uliofuata ambao Yanga walimaliza vinara.
Katika msimu huu, wakati Azam wakiibuka bingwa, Yanga imemaliza nafasi ya pili na Simba ikiangukia nafasi ya nne.
Hiki ni kitisho cha wazi kwa timu hizo kongwe kwani katika mazingira ya sasa, haitashangaza watani hao wakizikosa nafasi mbili za juu huko tuendako.
Kama kikosi cha Mbeya City chini ya Mwambusi kitabaki kama kilivyo hadi msimu ujao, kinaweza kufanya makubwa zaidi na kutwaa ubingwa ama kushika nafasi ya pil
Share this article :

Chapisha Maoni

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. bentabless.com - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger