ASKOFU wa Kanisa la Methodist
Jimbo la Dodoma, Joseph Bundala, amemtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,
William Lukuvi, atubu makosa yake ili asamehewe.
Lukuvi akiwa katika sherehe za
kumsimika Askofu Bundala, aliwataka waumini waukatae mfumo wa serikali tatu
uliopendekezwa katika rasimu ya katiba inayojadiliwa na wajumbe wa Bunge
Maalumu.
Alisema kama wananchi wakikubali
serikali tatu jeshi litashika madaraka na Zanzibar itaukaribisha utawala wa
Kiislamu na Waarabu.
Akizungumza na Tanzania
Daima jana, Askofu Bundala alisema kiongozi imara ni yule anayetubu makosa
yake, ili taifa liendelee kuwa na umoja, amani, ushirikiano na utulivu.
Alibainisha kuwa kwa bahati mbaya
dunia imejawa na viongozi wasioweza kutubu makosa wala kujiuzulu nyadhifa zao
wanapofanya mambo yanayozusha mtafaruku ndani ya jamii.
Alisema wakati Lukuvi akitoa
kauli ile, yeye (askofu), alijua italeta mtafaruku mkubwa ndani ya jamii
kwakuwa serikali mbili au tatu ni jambo lililo kwenye mjadala mkubwa ndani na
nje ya Bunge.
“Kujua kosa ni elimu, viongozi
wengi hawana elimu hii, na sisi viongozi wa dini kazi yetu kubwa ni kupigania
jambo hili lielewekwe kwa jamii,” alisema.
Alisema viongozi wanapaswa
kuchunga ndimi zao, ili matamshi wanayoyatoa yasisababishe mgawanyiko ndani ya
jamii.
“Nawaomba Watanzania wamsamehe
Lukuvi, mimi sikutarajia angezungumza kauli ile ambayo imezidisha mpasuko ndani
ya jamii, nilijua atazungumza mambo ambayo yangewaunganisha zaidi wananchi.
“Najisikia vibaya kuona kauli
iliyotolewa na kiongozi tuliyemualika katika kanisa letu imesababisha mvurugano
ndani ya jamii, nafikiri ni jambo jema kwa Lukuvi kuomba radhi,” alisema.
Wanasiasa kutumia makanisa
Askofu Bundala, alisema hakuna
ubaya kwa viongozi wa siasa kuhudhuria shughuli mbalimbali za kidini, lakini
jambo kubwa wanalopaswa kufanya ni kuchunga kauli zao, ili zisije zikazusha
mitafaruku.
“Hatuwezi kuacha kuwaalika kwenye
shughuli zetu, lakini wanapaswa kujikita katika maudhui yanayofanana na eneo
walilopo, masuala ya siasa wakafanye katika majukwaa yao,” alisema.
Mwenendo wa Bunge
Askofu Bundala, alisema haamini
kwamba kauli iliyotolewa na Lukuvi kanisani kwao ndiyo iliyochangia wajumbe
wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kususia vikao vya Bunge Maalumu
la Katiba.
Alisema tangu mwanzo vikao vya
Bunge Maalumu vilionekana kutawaliwa na mabishano, itikadi za kisiasa na
misimamo iliyosababisha misuguano mikubwa.
“Sote ni mashahidi Bunge Maalumu
halikuwa pamoja tangu wanaanza vikao vyao, kilichotokea pale kanisani kwetu
kilikuwa ni hitimisho tu, kama wangekuwa wanaendelea vizuri nina hakika
wangemkemea Lukuvi.
“Hawapo pamoja ndiyo maana hata
lilipotokea lile la Lukuvi wakaona ndiyo mlango wa kutokea, ninaamini UKAWA
watarejea bungeni baada ya kuzungumza na wenzao, hapa ni lazima wafanye
maridhiano kuilinda nchi,” alisema.
Awakaribisha UKAWA
Askofu Bundala, alisema anawaunga
mkono UKAWA kuamua kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya mchakato wa
katiba, lakini waifanye kazi hiyo kwa kutanguliza ukweli na si kuwarubuni
wananchi.
“Kama nia ni kutoa elimu tu, hilo
ni jambo la kheri kwa kuwa ni lazima wananchi wapate elimu, ili wakifikia hatua
ya kupiga kura ya maoni wajue kipi sahihi, UKAWA wakija kuturubuni
sitakubaliana nao hata kidogo,” alisema.

Chapisha Maoni