UMOJA
wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umetangaza vita kwa vyama vya siasa,
hususan kwa wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
UVCCM
imesisitiza kupambana na wajumbe wa UKAWA watakaotumia mikutano yao ya hadhara
kuwakashifu waasisi
wa Muungano, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Aman Karume.
Vita
hiyo ilitangazwa jana na Katibu Mkuu wa UVCCM, Paul Makonda, alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari juu ya mwenendo wa UKAWA kuendelea na
maandalizi ya mikutano yao nje ya Bunge.
Mbali
ya kuagiza UVCCM ichukue sheria mkononi, Makonda alivitaka vyombo vya dola
kuwachukulia hatua za kisheria wanasiasa aliodai wanasababisha uvunjifu wa amani
nchini.
Makonda
alisema iwapo vyombo vya dola havitawachukulia hatua watu hao, UVCCM
hawatakubali kuona Mwalimu Nyerere, mzee Abeid Aman Karume na Rashid Kawawa
wakitukanwa na kudhalilishwa hadharani.
“Hatutakubali
tena na ninaomba vijana wote wa ‘Green Guards’ wakae tayari popote watakapoona
waasisi wanatukanwa, wachukue hatua. Huu unyonge sasa basi.
“Sisi
kama Umoja wa Vijana tunajisikia vibaya sana tunapoona waasisi wa taifa letu
wanadhalilishwa na kutukanwa kwa kigezo tu cha kujenga hoja na kutafuta kuaminika
na kukubalika.
“Nimejaribu
kupitia kanuni zetu, kanuni ya 46 (e) ya Bunge Maalumu inasema ni
marufuku au hairuhusiwi kutumia jina la Rais wa Jamhuri ya Muungano, Rais wa
Zanzibar au marais wastaafu, kuwatumia kwa dhihaka au kwa kutaka kushawishi
hoja fulani iweze kukubalika, na hizi kanuni zimepitishwa na wajumbe wote
lakini kwa masikitiko makubwa, Mwalimu Nyerere ameonekana ni aliyezoea vya
kunyonga, kwa sababu nimeipitia ile ‘Hansard’ kwa umakini zaidi kuona maneno
ambayo alikuwa anatumia Mheshimiwa Tundu Lissu, ni maneno ya kufedhehesha na
wala si maneno yanayostahili kwa viongozi ambao wanaheshimika,” alisema.
Akizungumzia
kuhusu wapinzani kutoka ndani ya Bunge, alisema watu wenye hoja
hawakimbii bali hupambana kwa hoja.
“Leo
hii mnalisusa Bunge mnaenda kwa wananchi, mnaenda kuwaambia nini? Hapa
kinachotafutwa ni nchi yetu isitawalike,”
alisema.
Hata
hivyo Makonda katika taarifa hiyo amepotosha umma kwani Lissu hajawahi
kumkashifu wala kumtukana Mwalimu Nyerere wala mzee Karume.
Wakati
akitoa maoni ya watu wachache bungeni, Lissu alisema Mwalimu Nyerere ndiye
aliyeiua Tanganyika wakati hakuwa na mamlaka kisheria kufanya hivyo.
Sehemu
ya hotuba ya Lissu iliyokaririwa na gazeti hili
Lissu
alisema wajumbe wengi wamekuwa wakipotosha umma kwamba kukubali serikali tatu
ni kuvunja hati ya makubaliano ya muungano ambayo haipo wala haijawahi kutolewa
mbele ya hadhara.
“Swali
la msingi linalohitaji kuulizwa, je, hati hii ipo, swali la pili je, hati hii
ni halali? Swali la tatu, kama hati hii ipo na ni halali je, muungano huu ni
halali?,” alihoji.
Lissu
alisema hakuna ushahidi kwamba kuna hati ya muungano kwa kuwa hata
Umoja wa Mataifa kunakoelezwa ilipelekwa wamethibitisha hakuna jambo
hilo.
“Hati
ya Muungano haipo Zanzibar wala Tanganyika, haipo UN wala bungeni, sasa hiki
kilichozungumzwa na wengi kuwa kuanzisha muundo wa serikali tatu ni kuvunja
hati hizo ni uongo tu, zama za uongo sasa zimefikia mwisho.
“Nusu
karne ya uongo sasa ikome, tuambiane ukweli hivi sasa, waliozoea vya kunyonga
kamwe hawawezi vya kuchinja, mimi nawataka wajumbe wenzangu tufikie mwisho wa
kudanganya,” alisema.
“Ni
nani aliyeshuhudia wakati wa kutiliana saini makubaliano ya muungano? Hakuna
walioshuhudia, wale wote walioshuhudia jambo hilo waliuawa, sasa mnahofia nini
kuingia kwenye serikali tatu?” alihoji.
Bunge
la Tanganyika lilithibitisha kuungana na Zanzibar lakini Zanzibar haikuridhia
jambo hilo kwa mujibu wa nyaraka mbalimbali zilizopo.
Lissu
alisema nyaraka zinaonyesha kuwa Aprili 4, mwaka 1964 siku moja baada ya
muungano Mwanasheria Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Constantine Paulo, aliandika
barua kwa ubalozi wa Tanganyika akiwaambia wamesikia kuwa wameungana na
Zanzibar, wapeleke hati ya makubaliano hayo ili iweze kupata usajili wa Umoja
wa Mataifa itambulike kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
Alisema
Mei 6, mwaka huo huo siku kumi baadaye Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanganyika
ikapeleka tamko rasmi kwamba kweli wameungana na hati ya muungano,
wameiambatanisha na ‘noticefication.’
Aliongeza
kuwa Mei 14, wiki moja baadaye mwanasheria huyo akaandika ‘telex’ kwa serikali
Tanzania akiwataka Watanzania wawatumie nakala mbili za hati ya makubalino ya
muungano ili waisajili kwa mujibu wa ibara ya 102 ya United Nations Charter.
“Taarifa
hii inaamanisha kuwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania iliposema kwamba
tumewaleteeni hawakupeleka, sasa mwenyekiti ushahidi kwamba Umoja wa Mataifa
haujawahi kupelekewa hati ya muungano umepatikana Machi 3, 2009 wakati ofisa
habari za kisheria wa kitengo cha mikataba ya kitaifa wa Umoja wa Mataifa,
ofisi inayoshughulikia masuala ya kisheria alipomwandikia mtafiti mmoja
aliyeandika kitabu kwamba hakuna ushahidi wowote kwamba hati ya muungano
ilisajiliwa kwenye sekretarieti ya Umoja wa Mataifa.
“Kama
ingesajiliwa kungekuwa na hati ya usajili iliyoambatanishwa, nimeangalia hakuna
kitu kama hicho, Mwenyekiti, hati ya makubaliano ya muungano haipo Umoja wa
Mataifa na haipo Tanzania na kuna ushahidi kwamba haipo Tanzania,” alisema.
Alisema
mwaka 2005 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilishitakiwa Mahakama Kuu ya
Zanzibar na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Idd Pandu Hassan, aliambiwa apeleke
hati ya makubaliano ya muungano yenye saini ya Nyerere na Karume.
“Maneno
ya Mwanasheia Mkuu wa Zanzibar yanasema hivi kwa barua yake ya tarehe
22/6/2005, anasema; ‘ofisi yangu haikuweka kumbukumbu ya mkataba wa asili (original)
wa muungano wa Tangayika na Zanzibar tarehe 26/4/19964’” alisema.

Chapisha Maoni