KATIKA maisha ya kila siku
tunahimizwa kuwa tukipata tufurahi na tukikosa tutafakari.
Kushindwa kunafananishwa na giza
linalotangulia mbele ya mwanga wa kushinda, ambapo ndiyo mafanikio yenyewe
yalipo.
Juhudi kubwa ni kupambana na hilo
giza ili kufanikiwa kwa kujifunza, kushindana na kushinda kwa kuwa hakuna
mshindi pasipo mashindano.
Njia ya uhakika ya kutokushindwa
ni kudhamiria kushinda. Ni wazi kuwa jinsi unavyofikiria ndivyo
utakavyokuwa
kama msemo usemao: “Penye nia pana njia.”
Tatizo kubwa linalosababisha watu
wengi kutoyafikia mafanikio yao ni kukata tamaa.
Wengine huhisi kuwa wamepita njia
ambayo haijawafikisha kwenye malengo yao, jambo linalosababisha msongo wa
mawazo na wengine kuchanganyikiwa na kujikuta wakiongea wenyewe barabarani.
Kukata tamaa kunaleta uvivu wa
kutojishughulisha katika mambo ya kukuletea maendeleo, jambo linaloweza
kumfanya mtu kuwa tegemezi.
“Matumizi mabaya ya fedha ujanani
na kutojiwekea akiba ni maandalizi mabaya ya uzeeni,” huu ni msemo unaotumika
kuwahamasisha vijana na wenye umri wa makamo kufanya kazi kwa bidii na
kujiwekea akiba kwa ajili ya maisha yajayo kwani maisha fainali uzeeni.
Unapokata tamaa jiulize nani
anayejali? Jibu ni hakuna anayejali, hivyo cha msingi simama na uyashinde
maisha.
Itumie fursa uliyonayo katika
maisha yako. ‘Ukipiga picha’ ya kushindwa katika jambo lolote unalotaka kufanya
ujue unaelekea kushindwa.
Piga picha ya mafanikio utashinda
na amini kuwa umezaliwa kushindana si kushindwa. Jaribu kufanya kitu kizuri
unaweza kufanikiwa.
“Siku zote usifanye kitu kibaya
ili upate kitu kizuri, bali fanya kitu kizuri ili upate kitu kizuri zaidi,”
hayo ni maneno ya mwimbaji Mwasiti Almasi.
Wapo wanaoamini kuwa mafanikio
huletwa na bidii katika kazi na wengine huamini kuwa mafanikio ni majaliwa.
Katika maisha ya kila siku
unaweza ukawa umeshakutana na watu wanaoyashangaa maisha yao, wanashangaa kwa
sababu walikubali majaliwa yaliyowapeleka kwenye mafanikio.
Mafanikio katika maisha yanaanzia
kwenye mitazamo na fikra zilizoko ndani ya mtu, kile kilichoko ndani ya mtu
ndicho kitakachomhesabia mafanikio yake.
Mtazamo pekee ndio msingi wa
maisha kwa kuwa unachukua asilimia 64 ya nafasi katika maisha ya mtu.
Ni vema tukajifunza kutengeneza
mitazamo chanya ili tuweze kufanikiwa na njia mojawapo ya kutengeneza ni
kufikiria mema tu na kuacha kufikiria mabaya kwa sababu siri ya kushinda katika
maisha ni kuondoa fikra za kushindwa.
“ Mtu mmoja alikuwa akiishi kwa
kuuza maputo ya rangi nyekundu, njano, kijani na bluu. Aliyaweka nje ya duka
yakiwa yanapaa juu angani, watoto wengi walivutiwa na kuyanunua.
“Mauzo yake yakapanda juu sana,
siku moja akaja mtoto mdogo na kumuuliza yule muuzaji kuwa endapo angekuwa na
puto la rangi nyeusi nalo lingeweza kupaa angani.
“Muuzaji akamjibu kinachofanya
puto lipae angani si rangi yake bali kile kilichomo ndani…hivyo kinachotufanya
sisi tuwe juu ni mtazamo tulionao,” kinaeleza kitabu cha You Can Win
kilichoandikwa na Shiv Khera.
Umewahi kujiuliza kwanini watu au
kampuni nyingine zina mafanikio kuliko nyingine?
Hii si siri, hawa watu
wanafikiri na kufanya kazi vizuri, wamejifunza jinsi ya kuwekeza kwa watu wenye
mitazamo chanya. Mafanikio ya mtu, kampuni au nchi yanategemea sana ubora wa
watu wake.
Mfano kuna mnara mrefu,
maarufu kama Calgary Tower wenye urefu wa mita 190.8 na uzito wa tani
10,884; ambapo tani 6,349 iko chini ya ardhi ambayo ni sawa na asilimia 60 ya
jengo zima.
Hii ina maanisha kwamba majengo
marefu duniani yana misingi imara hata karibia uzito wa robo tatu ya jengo zima.
Kama iliyo kwa mnara mrefu na
mzuri duniani ulivyo na msingi imara, vivyo hivyo hata kwa binadamu yeyote
anapaswa kuwa na msingi imara.
Kitabu cha ‘You Can Win’
kinaeleza kwamba mkulima mmoja wa Afrika alikuwa na shamba kubwa na bado
alikuwa na maisha duni.
Siku moja akaja mtu mwenye busara
nyumbani kwake akamwambia kuwa iwapo mkulima huyo angepata almasi yenye ukubwa
sawa na kichwa chake angekuwa tajiri mpaka kufa kwake na watoto wake.
Huyo aliposikia hivyo haikupita
muda akauza shamba lake lote akasafiri kwenda nchi za nje na familia yake
kuitafuta almasi na kuinunua.
Alipofika huko akakuta pesa
aliyokuwa nayo ni ndogo haiwezi kununua almasi na alishaitumia kama nusu hivi
kwa gharama za kusafiria, kwa mawazo akaamua kujiua kwa kujitupa kwenye
mto.
Baada ya muda mfupi yule mtu
aliyeuziwa lile shamba akagundua kuwa kwenye shamba lile kulikuwa na mawe
yanayong’aa akayachukua kwenda kupima akakuta ni almasi akayauza na kuwa
tajiri.
Yule mtu mwenye busara aliposikia
habari hizo akaamua kwenda kumtembelea yule mkulima alipofika kwenye lile
shamba akamuulizia akaambiwa kuwa mkulima huyo alishaliuza shamba hilo kwa mtu
mwingine na akasafiri kuelekea mbali, yule mtu mwenye busara akasikitika sana.
Hadithi hii ya mkulima ina maana
kuu tatu; kwanza mtazamo wako unapokuwa sawa,utagundua kwamba unatembea kwenye
fursa, hivyo hatuhitaji kwenda popote kinachotakiwa ni kugundua nafasi hizo.
Pili; wakati unaposifia uzuri wa
majani ya upande wa watu wengine ujue kuna watu wengi wanayakubali majani
yaliyopo upande wako na wanatamani hata kufanya kazi na wewe, lakini kwa sababu
hauzingatii majani ya shamba lako unachukua muda mwingi kuangalia majani ya
shamba la mwenzako, hivyo unaweza kufa maskini usipokuwa makini.
Tatu; bahati haiji mara mbili
kwenye maisha, inayofuata inaweza ikawa nzuri zaidi au mbaya, lakini kamwe
haiwezi kujirudia, tambua hilo, watu wengi wanashindwa kutambua bahati zao na
fursa hata itakapobisha hodi au kuonyesha dalili.
Mitazamo yetu huwa inaonyesha
wazi ni nini tulichopanga kukifanya, kwa wenye mtazamo chanya inaweza kuwa ni
jiwe la mafanikio lakini wenye mitazamo hasi inawezekana likawa tofali.
Kampuni kubwa hazipimwi kwa
kiwango cha fedha walichonacho bali wanapimwa kwa mtazamo wao na ushirikiano
wao na jinsi ambavyo wafanyakazi katika kampuni hiyo wanavyojihisi wakati
wanafanya kazi.
Mfano, mwekezaji anaposema kuwa:
‘Siwezi kufanya hiki,’ kuna maana mbili; moja ni kwamba hajui jinsi ya kufanya
hicho kitu, pili, hataki kufanya hicho kitu.
Kama hajui jinsi ya kufanya hicho
kitu basi hilo ni jambo la kukosa ujuzi na kama hataki basi shida iko kwenye
mtazamo kwa maana ya kwamba hajali thamani ya hicho kitu. Hivyo tukubali
kubadilika katika mitazamo chanya.

Chapisha Maoni