Home » » Waislamu wamshukia Lukuvi

Waislamu wamshukia Lukuvi

Written By Unknown on Jumanne, 22 Aprili 2014 | 21:51

JUMUIYA na taasisi za Kiislamu nchini zimemtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi kujiuzulu haraka iwezekanavyo kutokana na kauli za uchochezi alizozitoa wakati wa sherehe za kumtawaza Askofu wa Kanisa la Methodist mjini DodomaHatua hiyo inatokana na madai ya Lukuvi kwamba endapo muundo wa serikali tatu utapitishwa nchi itapinduliwa na jeshi na
kwamba Chama cha Wananchi (CUF) Visiwani Zanzibar kinashirikiana na Jumuiya ya Kiislamu ya Uamsho kufanya vurugu za kupinga muungano.
Lukuvi pia katika kauli yake hiyo ambayo imelaaniwa na wananchi wengi huku askofu wa kanisa hilo akimtaka aombe
radhi na kutubu, alisema kuwa wanaotaka nchi yao (Wazanzibari) hawawezi kujitegemea, bali wanataka serikali tatu ili wapate nafasi ya kujitangaza kuwa nchi ya Kiislamu.
Akizungumzia kauli hizo jijini Dar es Salaam jana mbele ya waandishi wa habari, msemaji wa jumuiya na taasisi za Kiislamu, Rajabu Katimba, alisema kuwa serikali inatakiwa ikanushe kwa uwazi na kuwaomba radhi Waislamu na wananchi kwa ujumla juu ya madai hayo ya Lukuvi.
“Sisi hatukutarajia waziri mwenye mamlaka makubwa na aliyeaminiwa na rais na kumwakilisha Waziri Mkuu kutamka kauli chafu na za uchochezi, tena kanisani dhidi ya Waislamu na Taasisi ya Kiislamu ya Uamsho iliyosajiliwa kihalali.
“Kauli hizi zina nia ya kuleta chuki, kuwatia woga wananchi na hatimaye kuchafua amani na kuwanyima haki yao ya kikatiba ya kupendekeza muundo wa katiba wanayoitaka,” alisema Katimba.
Alisisitiza kuwa rasimu ya katiba ambayo Lukuvi anasema ikipita italeta matatizo, imetokana na utafiti wa maoni ya wananchi wa Tanzania Bara na Visiwani ili kuboresha muungano na kutatua kero mbalimbali zilizodumu kwa miaka 50.
“Kulikuwa na haja gani serikali kutumia mabilioni ya fedha katika jambo ambalo Lukuvi na chama chake tayari walishakuwa na mpango wao wa kuendelea na katiba iliyopo hivi sasa? Kitendo cha kusimama kwa niaba ya serikali katika madhabau ya kanisa na kueneza propaganda za uchochezi amepata wapi ushahidi juu ya taasisi zetu kuhusika na hayo?” alihoji.
Kitimba aliongeza kuwa kitendo cha kuwashambulia wanaoamini katika muundo wa serikali tatu ni kumdhalilisha Rais Jakaya Kikwete aliyeteua kwa umakini wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokusanya maoni ya wananchi.
“Kumekuwepo na taarifa za kuzusha kwamba mfumo huo wa serikali tatu ni mpango wa Uamsho ili Zanzibar iwe nchi ya Kiislamu. Huu ni uongo na upotoshaji,” alisema.
Katimba alitoa wito kwa viongozi wa dini na serikali kuacha kuwatisha na kuwakashifu wale wanaotoa maoni yao na kuonyesha kasoro za waliotangulia kwani wao hawakuwa miungu wasio na upungufu.

“Kwa kufanya hivyo ni kuzuia uhuru wa watu kutoa maoni yao, pia kuwafanya watu wasitamani kuishi kwa mawazo yanayoendana na maisha yao ya sasa wayatakayo na badala yake ni kuwalazimisha kuishi kwa mawazo na mtazamo wa waliopita,” alisisitiza Katimba.
Share this article :

Chapisha Maoni

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. bentabless.com - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger