MKAKATI wa
kuzima ndoto za Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa asigombee urais mwaka
2015 kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), umevuja, Tanzania Daima Jumatano
limedokezwa.
Kwa mujibu
wa kielelezo cha waraka wa mawasiliano ya wapinzani wa Lowassa, mkakati huo
unaongozwa na mtoto wa kigogo akishirikiana na Umoja wa Vijana (UVCCM) ambao
wanadaiwa kumuunga mkono mmoja wa mawaziri wanaotajwa kugombea urais.
Lowassa ni
mmoja wa makada wa CCM wanaotajwa kutaka kuomba kuteuliwa na CCM kuwania urais
mwaka 2015. Wengine ni
Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, Waziri wa
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick
Sumaye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano), Stephen Wassira na William
Ngeleja.
Katika
mawasiliano yao yaliyovuja na kusambazwa mitandaoni, mtoto huyo wa kigogo na
wenzake wanawashambulia kwa maneno makali Hussein Bashe na Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, kwamba ni vibaraka
wanaomdanganya Lowassa kuwa atakuwa rais wa nchi.
Kundi hilo
linajitapa kwamba hawawezi kuwapa vichaa nchi wakati uwezo wa kuongoza wanao na
kujiapiza kuwa kundi la Lowassa wakiingia Ikulu, wao watahama nchi.
“Ushindi
hapa ni Baraza moja kwa moja, ili tujipange mapema. Lazima tuweke majeshi sawa
tuweke historia Magogoni (Ikulu). Nilishakwambia mkuu, Lowassa haingii Ikulu.
“Anayemdanganya
ni wapambe, wakina Msomali Bashe. Hatutaki walevi Ikulu. Mtu alishakauka hata
kutembea hawezi, Ikulu ndio ataweza,” yanasomeka mawasiliano ya kundi hilo
ambayo yameambatana na matusi ya nguoni yasiyoandikika kitaaluma.
Katika
mawasiliano hayo, anashambuliwa pia January Makamba anayetajwa kuutaka urais,
lakini hapa anaelezwa kuwa kibaraka wa Lowassa anayebebwa na Rostam Azizi.
“Hao vijana
wa Lowassa wanaelekea kuzimu. Wakiingia Ikulu nahama nchi. Haiwezekani na
haitatokea. Halafu huyo mnafiki January ambaye anabebwa na shemeji yake Rostam
dawa yake inachemka.
“Muhimu sisi
kujipanga, lazima UVCCM iwe imara. Hatuwezi kuwapa vichaa nchi wakati uwezo
tunao wa kuongoza. Lazima tujiimarishe ndani na nje ili tushinde 2015,”
inasomeka sehemu ya mawasiliano hayo.
Itakumbukwa
UVCCM kupitia kwa Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi, Paul Makonda na wenzake,
wamekuwa wakitumika kumshambulia hadharani Lowassa, wakidai anaharibu chama kwa
sababu zake za kusaka urais.
Katika tamko
lao la mwisho, vijana hao kupitia Makonda ambaye ni mfuasi wa Membe, mmoja wa
wagombea urais watarajiwa kupitia CCM, walidai kuwa Lowassa hana sifa za kuwa
rais wala hafai kuwa amiri jeshi mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama.
Mkakati huo
wa kumshambulia waziwazi Lowassa, ambaye kundi lake limeonekana kuwa tishio
ndani ya CCM, ni uthibitisho tosha kwamba siasa za kuchafuana zinazidi kushika
kasi wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu 2015.
Licha ya
kutoweka wazi msimamo wa kundi analoliunga mkono, Tanzania Daima Jumatano
limedokezwa kuwa mtoto huyo wa kigogo anayemwandama Lowassa kwa kushirikiana na
UVCCM anampigania mmoja wa mawaziri ili awe mrithi wa Rais Jakaya Kikwete.
Mkakati huo
wa familia ya kigogo kumbeba waziri katika uchaguzi mkuu ujao, ulianzia tangu
wakati wa uchaguzi wa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) mwaka jana, kwa
kumpigania apate nafasi hiyo baada ya mambo kuwa yamemwendea vibaya.
Sasa
wapinzani hao wa Lowassa wakiongozwa na mtoto huyo wa kigogo, wameanza
kutapanya fedha kwa makada wao kwenye kata ili kusimika mizizi ya mtu wao
wanayemuunga mkono.
Kupitia
mawasiliano yao hayo yaliyofanyika Aprili 5, mwaka huu, mtoto huyo wa kigogo
anamwelekeza mwenzake namna ya kuchukua fedha mahala kwa mtu kwa ajili ya
kugawia wapambe wao.
“Usisahau
kupitia pale Mikocheni kwa … (anatajwa mtu), uchukue milioni 50 uje nazo,
ameishazitayarisha. Hakikisheni kila mtu wetu kwenye kata ameachiwa sh milioni
5, anzeni na … (anatajwa mtu mwingine),” yanaonyesha mawasiliano hayo.

Chapisha Maoni