RAIS wangu, siku chache
zilizopita, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta aliwatembelea
viongozi wawili wa dini,
Muadhama Polycarp Kardinali Pengo na Sheikh Mkuu wa Tanzania Mufti Shaban bin Issa Simba.
Muadhama Polycarp Kardinali Pengo na Sheikh Mkuu wa Tanzania Mufti Shaban bin Issa Simba.
Yaonekana viongozi hawa wawili kwake
ndio viongozi wa dini wa muhimu zaidi. Ni kweli kuwa wana waumini wengi zaidi.
Ukiwarubuni utawapata maamuma wengi.
Hakuwakumbuka hata viongozi wa
dini maswahiba wake waliokuwa wanamruhusu kuyatumia makanisa yao kama majukwaa
ya kulialia juu ya mahasimu wake katika kufanya ufisadi. Maongezi yao yalikuwa
ya siri.
Dunia imezoea kuona mambo yote ya
kishetani kufanywa gizani, huku yakigubikwa na usiri mkubwa! Mambo
yanayompendeza Mungu hufanywa kwa uwazi.
Sitta akitabasamu anasema
alikwenda kuwajulisha yanayotokea bungeni. Ah! Ni Mtanzania gani ambaye haoni
na kusikia utoto, upuuzi na mambo ya aibu yanayotokea bungeni?
Hadi wanatamani wajumbe wake ndio
wangekuwa abiria wa ndege ya Malaysia, wakazame baharini! Hawa watakuwa
viongozi gani ambao Sitta anataka kusema hawauoni ufedhuli unaotokea bungeni
hadi akawaeleze?
Rais wangu, madhali Sitta
ameshindwa kuwaambia wananchi kile alichowaeleza viongozi wa dini, basi
viongozi hao wawaambie waumini wao na wananchi kwa jumla ni nini Sitta
aliwaambia.
Wasipofanya hivyo heshima yao
katika jamii itakuwa shakani. Timamu watawaweka kundi moja na Sitta.
Rais wangu, Samuel Sitta kama
Adamu na Hawa walivyokula tunda walilokatazwa na Mwenyezi Mungu na hivyo
wakaifanya dunia kuwa mahali pa mateso hadi mwisho wa dunia, ndivyo alivyoifanya
nchi hii kuwa mahali pa mateso hadi leo kwa kupotosha hoja ya Richmond.
Waliwahukumu ambao hawakustahili
kuhukumiwa na wakawahifadhi waliostahili kuhukumiwa! Kuzuga wakazuka manabii wa
uongo waliohubiri kupandikiza chuki na fitina kati ya watu wa Mungu waliokuwa
wamezoea kuishi kwa upendo, amani na mshikamano.
Miaka miwili mfululizo makamanda
wa kishetani waliopanda majukwaani kuhubiri ufisadi wao, hakuna hata siku moja
waliosikika wakihubiri neno la amani, upendo na mshikamano miongoni mwa Watanzania.
Waliendelea kulialia hadi walipotunukiwa.
Kwa bahati mbaya masikini wa nchi
hii waliwasikiliza wana hawa wa shetani bila kugundua unafiki wao. Leo Sitta
hata malipo ya Dowans yamekuwa kama halali!
Nalikumbuka vizuri sasa gazeti
makini la MwanaHalisi. Liliandika kwa herufi kubwa, Sitta umeifunga kihuni hoja
ya Richmond bungeni, lakini kwa wananchi hoja ya Richmond haitafungwa!
Uhuni uliofanywa katika kuimaliza
hoja ya Richmond bungeni, ndio uliowaletea magumu masikini wa nchi hii hadi
leo, Masikini wa nchi hii wataendelea na maumivu ya Richmond hadi watakapoamka
kifikra na kuwaweka kikaangoni Sitta na wenzake ili wauseme ukweli waliouficha.
Ana deni kubwa mtu huyu kwa masikini wa nchi hii.
Rais wangu, Samuel Sitta
amepoteza fursa ya pekee alipokutana na viongozi wakuu wa dini. Kwa kuwa umri
wake umekwenda, angeitumia fursa hiyo kutubu mbele yao na mbele ya Mwenyezi
Mungu amsamehe kwa aliyoifanyia nchi hii siyo kuongeza mengine.
Baba Muadhama Polycarp Kardinali
Pengo naye akumbuke kuwa kauli ya kejeli ya ‘chaguo la Mungu’ ilianzia kanisani
kwake, nayo bado inakera waumini wake hadi leo. Asiongeze na hili.
Kufanya siri na watu wa aina hii
kunaongeza shaka na kuliumiza Kanisa la Mungu. Kanisa likiungana na watawala na
kuwaacha kondoo wa Bwana bila mchungaji mwema, Mungu hatakubali.
Atamtuma Baba Joseph Sinde
Warioba na wenzake kuwachunga hata kama hawatakuwa na fimbo ya kichungaji.
Tume aliyokuwa anaiongoza Baba
Warioba ni Tume ya Rais. Ndiyo kusema maoni ya wananchi yaliyokusanywa na Tume
ya Rais, yalikusanywa na rais mwenyewe.
Kwa kuwasilisha maoni ya watu wa
Mungu kama walivyoyatoa, Baba Joseph Sinde Warioba amejipatia thawabu kubwa
mbele ya Mwenyezi Mungu.
Thawabu ambayo angeistahili
muanzilishi. Lakini kama Waswahili wasemavyo, “Mwenyezi Mungu hamfichi
mnafiki”, mwenyewe kaikana!
Viongozi hawa wa dini,
waliishakaririwa wakishabikia serikali mbili kama CCM wanavyoshabikia.
Lakini nao kama CCM, hawasemi
serikali mbili katika nchi moja kama zilivyoachwa na waasisi wa Muungano
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Abeid Amani Karume.
Hawana ujasiri wa kuwaambia
watawala waifute nchi ya pili iliyojitokeza baada ya waasisi kufa ili kuondoa
utata. Wanatamani kuunganisha nchi mbili kwa serikali mbili, kitu ambacho hata
Nyerere na Karume hawakuweza.
Kutamani tu kuunganisha nchi
mbili kwa serikali mbili, wanasema kunaonyesha kama vile umeme unaoingia
kichwani ni mdogo.
Rais wangu, nawaomba waumini wa
dini zote, wanapowaona viongozi wao wa dini wanaambatana na wanasiasa wachovu,
waliopauka kisiasa kwa tamaa, wao wasiiharibu imani waliyonayo kwa Mungu wao.
Waendelee kuamini kuwa Mwenyezi
Mungu yupo. Na sisi wote tunaomtumikia ni stahili yetu kuitwa watumishi wa
Mungu. Hakuna mwenye haki ya kudai kuwa yeye ndiye mtumishi wa Mungu zaidi.
Kuwa kiongozi wa dini ni mpango
wa Mungu tu kuwa kila palipo na kundi kuwe na kiongozi. Ndiyo maana tuna
viongozi wa vikundi vya kisiasa, vya kiharakati na hata vya kigaidi.
Wanyama nao hata siafu wana
viongozi wao! Mwenyezi Mungu hana balozi wa kumwakilisha hapa duniani. Toka
manabii na mitume wapite hajamtuma mtu duniani kuja kumwakilisha.
Rais wangu, kama viongozi hawa
hawawezi kuwaambia waumini wao kile walichoambiwa na Sitta, basi wawaambie nini
wao walimwambia Sitta. Je, walimtaka awaeleze ilikuwaje Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba Jaji mstaafu Joseph Sinde Warioba awasilishe rasimu kabla
Bunge halijawa?
Kamusi ya Kiswahili sanifu kama
ilivyochapishwa na Oxford inatafsiri neno ‘zindua’ kuwa ni ‘anzisha’ au ‘fungua
kitu kwa mara ya
kwanza ili kianze kutumika’.
kwanza ili kianze kutumika’.
Hivyo kabla ya kuanzishwa
(kuzinduliwa) na rais, hapakuwapo na Bunge la Katiba. Baba Warioba
alilazimishwa kuwasilisha rasimu kwa kikundi tu cha watu ambao wahuni wachache
wamefanikiwa kulifanya kundi lote lionekane kama la wahuni tu.
Rasimu inayojadiliwa haijawasilishwa
rasmi bungeni! Huu ni uhuni. Je, ndiyo huu uhuni waliokuja kujulishwa viongozi
wetu wa dini? Lakini je, walimkanya asichakachue maoni ya wananchi kwenye
rasimu?
Rais wangu, achana na wanasiasa
hawa ambao muda wao wa kutumika umekwisha. Mikakati wanayoifanya inawaongezea
hasira tu wananchi.
Busara sasa ni wewe kumsikiliza
Katibu Mkuu wako Abdulrahman Kinana kule vijijini anakohangaika na shida za
masikini wako. Anajenga, hawa wanabomoa! Siku za hukumu zinakuja, hawa
hutawaona!
Chapisha Maoni