Dar es Salaam. Rais Jakaya
Kikwete ameendelea kusisitiza kuwa Tume ya Jaji Joseph Warioba haina ushahidi
kwamba Watanzania wengi wanataka muundo wa Muungano wa serikali tatu.
Kauli hiyo aliitoa wiki hii
jijini Dar es Salaam kwenye
mahojiano maalumu na Kituo cha Televisheni cha NTV
kilichopo chini ya Nation Media Group (NMG).
Rais Kikwete ambaye moja ya mambo
atakayokumbukwa kwenye uongozi wake ni kuasisi mchakato wa Katiba, alizungumzia
hoja ya serikali tatu akisema, hakuna ushahidi kwamba Watanzania wengi wanataka
muundo wa Muungano wa serikali tatu.
“Hakuna ushahidi kwamba watu
wengi katika nchi hii wanataka serikali tatu, hakuna ushahidi wa namna hiyo,
hata tume yenyewe haikubaini hicho. Kinachofanywa na vyombo vya habari ni
kuandika habari za wajumbe wa Bunge la Katiba wanaotaka serikali tatu, ndiyo
kwenye masilahi yao, wanapaza sauti za wale wanaotaka serikali tatu, hao ndiyo
sauti zao zinasikika. Lakini hawataki kupaza sauti za wale wanaotaka serikali
mbili,” alifafanua.
Hii ni mara ya pili kwa Rais
Kikwete kuikosoa ripoti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji
Joseph Warioba. Mara ya kwanza aliikosoa wakati akizindua Bunge la Katiba Machi
21 mjini Dodoma.
Rais Kikwete ambaye amewahi kuwa
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa kipindi cha miaka 10,
katika mahojiano hayo alisema katika kuadhimisha miaka 50 ya Muungano, jambo
muhimu na kubwa ni kuendelea kuwapo kwa Muungano.
“Tunayo mifano ya nchi
zilizojaribu kuungana, lakini zilishindwa, Senegal-Gambia, Ghana-Guinea, Misri
na Libya.
“Muungano umeendelea kuwepo kwa
nusu ya karne ni mafanikio makubwa. Kumekuwepo na wakati mgumu na changamoto
mbalimbali, lakini tumeweza kukabiliana nazo na umeendelea kuwa imara zaidi.
Siyo kuendelea kuwepo tu pia umeendelea kuimarika na mchakato wa mabadiliko ya
Katiba utaimarisha zaidi Muungano na tutakuwa na Muungano imara baada ya kupata
Katiba Mpya,” alifafanua Rais Kikwete.
Akizungumza kwa kujiamini
kutokana na uzoefu wake wa muda mrefu ndani ya CCM na Serikali, Rais Kikwete
alisema Muungano ulikotoka ulikuwa imara na umeendelea kukua katika hali ya
uimara wake.
“Kuna mambo ambayo tumefanya
yamezidi kuimarisha Muungano na umeendelea kuwa na mafanikio makubwa.”
Alisema suala si kuendelea kwa
muundo ulivyo sasa, suala la msingi ni kujadili namna ya kutengeneza muundo wa
Muungano, kwamba upi ni bora.
Rais Kikwete: “Mimi ni mmoja wa
wanaoamini kwamba muundo wa serikali mbili ni bora zaidi kwetu. Siyo suala la
kuendeleza hali iliyopo, ni muhimu kubadilika kama kuna sauti zinazotaka kubadilika
na pia kama kuna hoja nzito ya kutaka mabadiliko, lakini sioni kama Muungano wa
Serikali tatu ni hoja nzito ya kufanya mabadiliko, itasababisha matatizo
mengine na mwisho kusababisha muungano kuvunjika.”
Rais Kikwete ambaye katika uzoefu
wake wa kazi za kisiasa amewahi kufanya kazi Zanzibar, alisema alipoingia
madarakani mwaka 2005 hoja kuu ilikuwa ni kutatua mzozo wa kisiasa uliokuwa
ukiendelea kwa muda mrefu kati ya vyama vya CUF na CCM visiwani humo.
Alisema: “Tumeweza kuutatua na
sasa tuna Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Kabla ya hapo kulikuwa na matatizo
mengi, wakati wa uchaguzi mambo yanatulia, ukimalizika uchaguzi kunazuka
matatizo ya kisiasa, tukaamua kuvileta vyama hivi pamoja tukafanya mjadala wa
kina na uamuzi uliofikiwa ni kuwa na serikali ya umoja wa kitaifa, na sasa
Zanzibar kuna utulivu wa kisiasa.”
Rais Kikwete akizungumzia suala
la Muungano alisema wakati wa Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, aliunda
tume, Tume ya Shelukindo (iliongozwa na William Shelukindo) kuangalia kero za Muungano
na walikuja na kero 31.
Alisema alipoanza kazi mwaka 2006
kero za Muungano zilikuwa zimebaki 13, akashughulikia kero tisa, zimebaki kero
nne tu.
Rais Kikwete alisema kimsingi
uhuru wa vyombo vya habari kwa Tanzania ni mpana na kwamba hata gazeti lililofungiwa
ni moja na mengine yalifungiwa kwa muda tu.
Alisisitiza kwamba habari za
kuchochea majeshi kufanya mapinduzi, habari za kuchochea vijana kuleta vurugu
hatazivumilia, na kwamba chombo cha habari kitakachojielekeza kwenye habari za
namna hiyo kitafungiwa.
“Wakiandika Rais Kikwete nchi
imemshinda hainipi tabu, kwa kuwa najua nchi haijanishinda,” alisema Rais
Kikwete huku akitoa mfano wa namna redio Mille Collines ya Rwanda ilivyochangia
mauaji ya halaiki nchini humo.
Rais Kikwete alitoa mfano mwingine
wa namna vyombo vya habari vilivyochangia uvunjaji wa amani ni mwandishi wa
habari wa Kenya ambaye amefunguliwa mashtaka ya uhalifu wa kimataifa katika
Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), iliyopo The Hague nchini
Uholanzi.
Mwandishi wa habari
aliyefunguliwa mashtaka ICC ni mtangazaji wa Kituo cha Redio ya Kass FM, Joshua
arap Sang. Rais Kikwete huku akicheka alimuhoji mtangazaji wa NTV “Unataka
habari kama hizo tuzivumilie?”
Kuhusu rushwa, Rais Kikwete
aliitaja idara ya mahakama kuwa ni moja ya changamoto na wiki iliyopita
alizungumza na Jaji Mkuu kuona namna gani wanaweza kuboresha, kuongeza mafunzo
kwa wapelelezi au waendesha mashtaka, kutokana na watuhumiwa wengi wa rushwa
kuachiwa huru.
Kuhusu uchumi, Rais Kikwete
ambaye amewahi kuwa Waziri wa Fedha alisema kinachofanyika ni kuimarisha uchumi
mkubwa, na kwa mujibu wa wachumi, uchumi wa nchi ukikua kwa asilimia saba
katika kipindi cha miaka 10, pato la taifa huongezeka mara mbili na uchumi wa
Tanzania umekuwa ukikua kwa asilimia saba kwa kipindi hicho.
Akizungumzia uhusiano wake na
Rais Paul Kagame wa Rwanda, Rais Kikwete alisema hana mgogoro na kiongozi huyo,
alichokifanya ni kutoa ushauri kuhusu namna ya kutatua migogoro ndani ya nchi
yao, ni hiari yao kufuata ushauri wake.

Chapisha Maoni