Dar es Salaam. Aliyekuwa
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba amesema baadhi ya wajumbe wa Bunge
Maalumu la Katiba wametumia vibaya Bunge hilo kwa kumshambulia na kumsingizia
mambo ya uongo kwa makusudi, akisema matusi yanayotolewa dhidi yake
yanamuumiza.
Kauli hiyo ya Jaji Warioba
imekuja wakati baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na viongozi wa CCM
wakiikosoa Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba kwa maneno makali,huku wakimshutumu
na kumkejeli yeye na baadhi ya wajumbe wa tume aliyoiongoza.
Akizungumza kwa mifano katika
mahojiano na gazeti hili jana, Warioba alisema kuwa anawashashangaa wajumbe hao
na viongozi wa CCM kwa kuacha kuijadili Rasimu ya Katiba, badala yake
wanamkosoa yeye na kumsingizia maneno yasiyo ya kweli.
“Bulembo (Abdallah Bulembo mjumbe
wa Bunge na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM) amenitukana, amenitukana…
amesema niliwahi kupokea rushwa huku akijua kabisa kuwa ni uongo. Yeye ni
kiongozi wa Kamati Kuu ya CCM, anasema uongo akijua ni uongo. Kwanza mimi
simjui wala sijawahi kumwona huyu mtu naambiwa tu anatoka Mara,” alisema Jaji
Warioba kwa sauti ya upole iliyoashiria kuumizwa.
Aliongeza kwamba siyo mara ya
kwanza kwa Bulembo kumshambulia kwa lugha za matusi, kwani aliwahi kufanya
hivyo tena kwenye moja ya mikutano ya CCM mkoani Tanga.
“Alifanya hivyo Tanga,
anachokifanya siyo kitu cha mzaha kwa sababu anafahamu kilichotokea,” alisema.
Akizungumzia kauli aliyoitoa
Waziri Hawa Ghasia wakati akichangia mjadala wa Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba
aliyemtaka Jaji Warioba kufunga mdomo kutokana na kazi yake ya kuwasilisha
Rasimu kumalizika, Jaji Warioba alisema: “Wao wanataka waseme uongo, mtu
mwingine asiseme kitu.”
Warioba alieleza kuwa tangu lugha
za matusi na kejeli zilipoanza kutolewa dhidi yake, baadhi ya watu walimshauri
kwenda mahakamani kufungua kesi, lakini alikataa kwa kile alichodai kuliheshimu
Bunge.
Alisema Bunge ndiyo lenye mamlaka
ya kufuatilia na kudhibiti kauli zinazotolewa bungeni, kama wahusika hawafanyi
hivyo hawezi kuchukua hatua yoyote.
“Kama kinga ya Bunge inatumika
vibaya unafikiri mimi nitafanya nini? Sina nia ya kuchukua hatua, watu
walipendekeza niende mahakamani, kuna wanasheria walisema hata nisipokwenda,
wao watakwenda mahakamani nikawazuia,” alisema Warioba ambaye pia ni Waziri
Mkuu mstaafu.
Akisimulia kuhusu uchaguzi wa
ubunge wa mwaka 1995 ambapo aligombea na kutuhumiwa kupokea rushwa na kufungiwa
kwa miaka minne, Warioba alisema taarifa hizo siyo sahihi kwa kuwa aliyepokea
rushwa ni aliyekuwa mgombea kwa tiketi ya NCCR Mageuzi (wakati huo), Stephen
Wassira ambaye sasa yuko CCM na ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na
Uratibu.
“Uchaguzi ule ulikuwa umejaa sana
rushwa, tukaenda mahakamani, Wassira akafungiwa asigombee,” alisema.
Akizungumzia maadhimisho ya
sherehe za miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Warioba alisema:
“Mimi ni muumini wa muungano, kwa miaka 50 taifa limekaa kwa amani, mshikamano
na umoja. Ni kweli tumekuwa na matatizo lakini yanaweza kutafutiwa ufumbuzi.”

Chapisha Maoni