Katibu Mkuu Kiongozi (KMK), Balozi Ombeni Sefue alilieleza
gazeti la mwananchi kuwa kwa hali ya mchakato huo ilivyo sasa, wameshindwa
kufikia lengo hilo, lakini hawajakata tamaa kuhusu kupatikana Katiba Mpya ndani
ya mwaka huu.
Ikulu imeeleza kuwa imeshindwa
kutimiza ahadi yake kwa taifa ya kulipatia Katiba Mpya ifikapo Aprili 26, 2014.
Kweli matarajio ya awali yalikuwa
hayo, lakini kama unavyoona hali ilivyo, ni vigumu kusema matarajio mengine,
ingawa majadiliano yaliyofanywa mwaka huu ni lazima Katiba inayopendekezwa
iwasilishwe kwa wananchi na mwakani tutakuwa na Katiba Mpya,” alieleza Balozi
Sefue.
Katika hali isiyoeleweka Balozi
Sefue alisisitiza msimamo wa awali wa Serikali kwamba Katiba itakayopatikana
itatumika kwenye Uchaguzi Mkuu, unaotarajiwa kufanyika mwaka ujao.
Dk Slaa
Katibu Mkuu wa Chama cha Maendeleo
na Demokrasia (Chadema), Dk. Willbroad Slaa, alisema hilo ni fundisho kwa
Serikali kwamba kiburi na jeuri havitakiwi katika masuala yanayohusu umma.
Alisema muda huo wa kupatikana
Katiba Mpya ulipotangazwa, walioanzisha kilio cha kudai Katiba Mpya nchini
ambao aliwataja kuwa ni vyama vya upinzani vya siasa, taasisi mbalimbali za
kijamii walipinga na kutoa ushauri kwa Serikali, lakini walipuuzwa.
Dk. Slaa alisema walipendekeza
kwamba badala ya kupeleka mchakato wa Katiba mchakamchaka, warekebishe kwa mara
ya 15 Katiba inayotumika, ili iende na wakati wa sasa ikiwamo Uchaguzi Mkuu
ujao kwa lengo la kutoa muda wa kutosha kwa mchakato wa taifa kupata Katiba
Mpya.
“Lakini walitukebehi na kututukana
sana, sasa kiko wapi Aprili 26 hiyo hapo na Katiba haijapatikana na kusema
itapatikana mwaka huu na kutumika kwenye Uchaguzi Mkuu mwakani ni ndoto za
mchana,” alieleza Dk. Slaa.
Dk. Slaa alisema tukio hilo liwe
fundisho kwa Serikali, wawe wakweli, wanyoofu na wafahamu kuwa nje ya Serikali
kuna watu makini na wanaojua vilivyo mchakato wa Katiba.
Alisema ana taarifa za Bunge
Maalumu kuahirishwa Mei 9, 2014 ili kupisha Bunge la Bajeti. Hivyo mategemeo ya
Katiba Mpya kwenye Uchaguzi Mkuu ujao, yanatia shaka.
“Kwa akili ya kawaida tu
isiyohitaji elimu ya chuo chochote, kutumia Katiba Mpya kwenye Uchaguzi Mkuu
ujao ni jambo lisilowezekana kwa hiyo waache kutuletea matumaini yasiyokuwapo,
sisi siyo watoto wadogo,” alieleza Dk. Slaa.
Kauli ya LHRC
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk.
Helen Kijo Bisimba, alisema siyo tu Serikali imeshindwa kutimiza ahadi ya muda
iliyojiwekea, bali hata mchakato wenyewe haueleweki.
Dk. Bisimba alisema kwa hali
ilivyo, hawana hakika ya kupata Katiba na ikipatikana haitakidhi matakwa ya
wananchi, kwa kuwa wanataka Katiba ya watu siyo ya kundi moja la watu.
“Mambo ya nchi hii tunayafahamu,
inaweza ikapatikana kwa nguvu lakini wajue wananchi wataikataa na hata
ikilazimishwa, haitakidhi mahitaji, itaweza kuathiri ustawi wa taifa,” alieleza
Dk. Bisimba.
Alisema hilo waliliona mapema,
wakataka kila hatua ya mchakato ipewe muda wa kutosha kabla ya hatua nyingine,
ili wananchi waelimishwe lakini hawakusikilizwa.Alisema kuwa katika mazingira
hayohayo, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilifanya kazi kubwa hadi kufanikisha
maoni ya wananchi kupatikana na kutengeneza Rasimu ya kwanza na ya pili
iliyowasilishwa bungeni Machi 18, 2014, lakini kwa jinsi Bunge Maalumu
linavyoendeshwa, kuna kila dalili kwamba kazi hiyo itaharibiwa.
“Wakichezea Rasimu wajue wanachezea
maoni ya wananchi, wanaoweza kuyakataa kupitia kura ya maoni na hivyo
kusababishia taifa hasara isiyomithilika,” alieleza Dk. Bisimba.
Dk. Bisimba alisema mchakato huo
umegharimu taifa fedha nyingi, muda mwingi, nguvu, akili, afya na hata uhai wa
watu, hautakiwi kufanyiwa mzaha.
Alipotafutwa Waziri wa Katiba na
Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro ili kuzungumzia suala hilo jana hakupatikana,
lakini Naibu Waziri wa wizara hiyo Angela Kairuki, alisema kuwa kwa hali ilivyo
ni dhahiri haiwezekani kupata Katiba Mpya kwa muda huu tofauti na ilivyodhaniwa
awali.
Hata hivyo, Kairuki alisema hawezi
kuzungumzia hatua iliyofikiwa katika mchakato huo kwani mwenye mamlaka ya
kuzungumzia ratiba ya Bunge Maalumu la Katiba ni mwenyekiti wake, Samuel Sitta.
“Hata hivyo tunachotakiwa
kuzungumzia ni ubora wa kazi inayofanyika ili kufikia lengo la kupata Katiba
itakayoongoza nchi kwa miaka 50 ijayo,” alisema Kairuki.
Chapisha Maoni