Mbeya. Maji ya kuwasha, mabomu na risasi za moto jana zilirindima jijini hapa kwa takriban saa mbili mfululizo, kutokana na waendesha bodaboda kuwazuia polisi waliokuwa wakimwokoa mtu anayedaiwa kushiriki njama za kumuua mwendesha pikipiki mwenzao, Zizza Mwambenja juzi.
Maeneo yaliyoathiriwa na vurugu hizo ni Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA) Tawi la Mbeya, Mitaa ya Iyela na Airport ambako watu walionekana wakikimbia ovyo.
Waendesha pikipiki hao walitaka kumkamata mke wa marehemu Mwambenja wakimtilia shaka kushiriki katika njama za kumuua kwa vile walikuwa na mgogoro wa kindoa na mwanaume aliyekuwa amekimbia kwenye nyumba yao.
Kamanda Msangi alisema kuwa waendesha bodaboda walivamia eneo la msiba jana, wakitaka kumhoji mke wa marehemu.
Alieleza kwamba waendesha pikipiki hao walidai kuuawa kwa Mwambenja kunamhusisha mke wake kwa vile ndoa yao ilikuwa kwenye mgogoro na kwamba zilikuwapo kauli za kumtishia maisha.
Katika harakati hizo, raia wema walipiga simu polisi kumwokoa na kwamba polisi walifika na gari lao walilitumia kumbeba.
Lakini, vijana wa bodaboda walipigiana simu na kupanga mawe eneo la barabara inayotoka eneo la tukio kabla ya kufika Mtaa wa Mafiati.

Chapisha Maoni