Mzozo wa kidiplomasia unanukia
kati ya Kenya na Somalia baada ya polisi kumkamata kimakosa mmoja wa maafisa
wakuu wa ubalozi wa Somalia nchini Kenya Siyad Mohamud Shire .
Tayari balozi wa Somalia nchini
Kenya Mohamed Ali Nur ameitwa na serikali yake kueleza matukio yanayoambatana
na kukamatwa kwa raiya wa asili ya kisomali ambao serikali inasema baadhi
yao
hawana vibali vya kuishi nchini.
Maafisa wa polisi nchini Kenya
wamekuwa wakiendelea na msako wao dhidi ya wahamiaji haramu na wale
wanaoshukiwa kushiriki matendo ya kigaidi na uhalifu.
Hata hivyo serikali ya Somalia
imesikitishwa nao kwa kumkamata afisa wa ubalozi wa Somalia anayeshughulikia
masuala ya kisiasa Siyad Mohamud Shire .
Kwa sababu hiyo Somalia imetuma
taarifa katika vyombo vya habari ikisema kuwa waziri mkuu Abdiweli Sheikh Ahmed
amefanya mazungumzo na balozi wa Somalia nchini Kenya aliyefika Mogadishu hapo
Jumapili kumweleza hatma ya raiya wa Somalia wanaoishi Kenya katika msako
unaoendelea
Japokuwa serikali ya Kenya
kupitia kwa wizara ya usalama wa kitaifa imekuwa ikishikilia kuwa hailengi
jamii yoyote katika kuwakamata raiya wa kigeni na kuwarejesha katika nchi zao
ama kambi za wakimbizi.
Taarifa hiyo imeanusha hilo na
kusema maafisa wa polisi wamekuwa wakiwazuilia wasomali wengi na kuwatesa.
Tukio la kumnasa, Bwana Siyad
Mohamud Shire limechukuliwa na serikali ya Somali kuwa ukiukaji mkubwa wa
mkataba wa kidiplomasia.
Inasemekana kuwa bwana Shire
alikamatwa na kuzuiliwa na polisi kwa muda licha ya kuwa na kitambulisho cha
kazi.
Mkutano kati ya waziri mkuu wa wa
Somali na balozi wa Kenya ulifanyika baada ya baraza la mawaziri kuandaa kikao
kisichokuwa cha kawaida kujadili hali ilivyo Kenya.
Juhudi za kumpata waziri wa mambo
ya nje wa Kenya balozi Amina Mohamed kueleza msimamo wa serikali hazikufaulu
ila maafisa wa polisi walikataa kuzungumzia suala hilo wakisema kuwa
litashughulikiwa na ngazi ya juu.
Polisi nchini Kenya walianza
msako kote nchini wiki tatu zilizopita baada ya matukio mengi
yanayoambatanishwa na ugaidi ama uhalifu kutokea huku zaidi ya watu kumi
wakifariki baada ya milipuko kadhaa kutokea katika mtaa wa Eastleigh na maeneo
jirani jijini Nairobi.
Kisichojulikana kwa sasa ni namna
nchi zote mbili zitakavyoendelea kushirikiana kidiplomasia katika mazingira
yaliyopo.

Chapisha Maoni