MAKOMBORA ya maneno yaliyokuwa yakitolewa na msemaji wa taarifa ya wachache bungeni, Tundu Lissu, juu ya muundo wa muungano, na kutokuwapo kwa Hati za Muungano kumetikisa serikali ambayo sasa imeamua kuzitoa hadharani hati hizo.
Huku akikatishwa mara kwa mara na taarifa na miongozo kutoka kwa baadhi ya wajumbe waaumini wa serikali mbili, Lissu alisema wajumbe wengi wamekuwa wakipotosha umma kwamba kukubali serikali tatu ni kuvunja hati ya makubaliano ya muungano ambayo haipo wala haijawahi kutolewa mbele ya hadhara.
“Swali la msingi linalohitaji kuulizwa, je, hati hii ipo? Swali la pili, je, hati hii ni halali? Swali la tatu, kama hati hii ipo na ni halali je, Muungano huu ni halali?”
Lissu alisema hakuna ushahidi kwamba kuna hati ya muungano kwa kuwa hata Umoja wa Mataifa, kunakoelezwa ilipelekwa, wamethibitisha hakuna jambo hilo.
“Hati ya Muungano haipo Zanzibar wala Tanganyika, haipo UN wala bungeni, sasa hiki kilichozungumzwa na wengi kuwa kuanzisha muundo wa serikali tatu ni kuvunja hati hizo ni uongo tu, zama za uongo sasa zimefikia mwisho.
“Nusu karne ya uongo sasa ikome, tuambiane ukweli hivi sasa, waliozoea vya kunyonga kamwe hawawezi vya kuchinja, mimi nawataka wajumbe wenzangu tufikie mwisho wa kudanganya.
“Ni nani aliyeshuhudia wakati wa kutiliana saini makubaliano ya muungano? Hakuna walioshuhudia, wale wote walioshuhudia jambo hilo waliuawa, sasa mnahofia nini kuingia kwenye serikali tatu?” alisema.
Bunge la Tanganyika lilithibitisha kuungana na Zanzibar lakini Zanzibar haikuridhia jambo hilo kwa mujibu wa nyaraka mbalimbali zilizopo.
Lissu alisema nyaraka zinaonyesha kuwa Aprili 4, mwaka 1964 siku moja baada ya muungano, Mwanasheria Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Costantine Paulo, aliandika barua kwa Ubalozi wa Tanganyika akiwaambia wamesikia kuwa wameungana na Zanzibar wapeleke hati ya makubaliano hayo ili iweze kupata usajili wa Umoja wa Mataifa, itambulike kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
Alisema Mei 6, mwaka huo huo siku kumi baadaye Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanganyika ikapeleka tamko rasmi kwamba kweli wameungana na hati ya muungano wameiambatanisha na ‘noticefication’.
Aliongeza kuwa Mei 14, wiki moja baadaye mwanasheria huyo akaandika ‘telex’ kwa serikali ya Tanzania akiwataka Watanzania wawatumie nakala mbili za hati ya makubaliano ya muungano ili waisajili kwa mujibu wa ibara ya 102 ya United Nation Charter.
“Taarifa hii inamaanisha kuwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania iliposema kwamba tumewaleteeni, hawakupeleka sasa mwenyekiti ushahidi kwamba Umoja wa Mataifa haujawahi kupelekewa hati ya muungano umepatikana Machi 3, 2009, wakati ofisa habari za kisheria wa kitengo cha mikataba ya kitaifa wa Umoja wa Mataifa, ofisi inayoshughulikia masuala ya kisheria alipomwandikia mtafiti mmoja aliyeandika kitabu kwamba hakuna ushahidi wowote kwamba hati ya muungano ilisajiliwa kwenye sekretalieti ya Umoja wa Mataifa.
“Kama ingesajiliwa kungekuwa na hati ya usajili iliyoambatanishwa, nimeangalia hakuna kitu kama hicho Mwenyekiti, hati ya makubaliano ya muungano haipo Umoja wa Mataifa na haipo Tanzania na kuna ushahidi kwamba haipo Tanzania,” alisema.
Alisema mwaka 2005 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ilishitakiwa Mahakama Kuu ya Zanzibar na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Idd Pandu Hassan, aliambiwa apeleke hati ya makubaliano ya muungano yenye saini ya Nyerere na Karume.
“Maneno ya Mwanasheia Mkuu wa Zanzibar yanasema hivi kwa barua yake ya tarehe 22/6/2005, anasema; ‘ofisi yangu haikuweka kumbukumbu ya mkataba wa asili (original) wa muungano wa Tangayika na Zanzibar tarehe 26/4/19964’” alisema.
Serikali kutoa hati
Baada ya makombora ya Lissu, Mwenyekiti wa Kamati Namba Sita, Stephen Wassira, alisema hati ya Makubaliano ya Muungano ya Tanganyika na Zanzibar iliyosainiwa na waasisi wa Muungano, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Aman Karume, ipo salama na itawasilishwa katika Bunge Maalumu la Katiba ndani ya siku mbili zijazo.
Baada ya Wassira kusimama alisema hapo wanazungumza na Watanzania na hivyo si vizuri kuzungumza mambo ya uongo.
“Mheshimiwa Mwenyekiti napenda kukuthibitishia kuwa Hati ya Makubaliano ya Muungano ipo na ipo imehifadhiwa sehemu salama kwa muda wote wa miaka 50 ya Muungano kwa niaba ya dola ya Tanzania, naomba kukuthibitishia kuwa Hati hiyo ya Muungano itawasilishwa kwenye Bunge baada ya siku mbili,” alisema Wassira.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amesema kuwa ametumiwa nakala ya hati ya muungano kwa nukushi (fax), kutoka Ikulu, Dar es Salaam na kwamba ataikabidhi kwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta.
Alibainisha kuwa nakala nyingine italetwa ikiwa imesainiwa na mwanasheria kuthibitisha uhalali wa nakala hiyo.
Mara baada ya taarifa hiyo, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta, alisema akiipata Hati ya Muungano iliyothibitishwa ataigawa kwa kila mjumbe ili waendelee vizuri na majadiliano.

Chapisha Maoni