Dodoma. Mjumbe wa Bunge la
Katiba, David Kafulila jana aligeuka shujaa bungeni na kubebwa juujuu na
wajumbe wenzake kutoka kundi la walio wachache baada ya ‘kusambaratisha’ hoja
za wajumbe wanaopinga Serikali tatu.
Kafulila ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kusini
(NCCR-
Mageuzi), alifanya hivyo alipokuwa akifafanua hoja kutoka kundi la walio wachache katika Kamati Namba Tano.
Mageuzi), alifanya hivyo alipokuwa akifafanua hoja kutoka kundi la walio wachache katika Kamati Namba Tano.
Miongoni mwa hoja ambazo alizijibu na kushangiliwa na
wajumbe, ni juu ya gharama za Serikali tatu, kuwa zitavunja Muungano, kwamba
Serikali ya Muungano itakosa mapato, hoja ya kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere na
uhalali wa takwimu za Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Alisema hoja kuwa Serikali tatu ni kuvunja Muungano si za
kweli, akisema ni propaganda zilezile ambazo CCM ilizitumia mwaka 1992 kutembea
nchi nzima kupinga mfumo wa vyama vingi.
“Wakati ule CCM ilitembea nchi nzima huku wakionyesha
video kuwa vyama vya upinzani vitaleta vita, lakini leo miaka 20 baada ya
kukubali mfumo wa vyama vingi hakuna vita vilivyoletwa na upinzani,” alisema
Kafulila. Alisema haiwezekani tume zote ambazo zinaundwa na Serikali
zipendekeze serikali tatu na kila wakati serikali iliyopo madarakani ikatae.
“Hoja ya serikali tatu siyo hoja ya Warioba, tume zote
zilizowahi kuchunguza muundo ya Muungano zote zilipendekeza serikali tatu,”
alisema na kuongeza: “Ofisi ya Rais ilipendekeza serikali tatu, ofisi ya Waziri
Mkuu ilipendekeza serikali tatu, inatuwia vigumu ndani ya muda mfupi, vyombo
hivi vibadilike na kutaka serikali mbili.”
Alisema wanaotaka serikali tatu wanataka kwa namna ambayo
inaimarisha Muungano, tofauti na maoni ya walio wengi kuwa serikali ya Muungano
itakuwa legelege kwa kuwa itakosa nguvu za kiuchumi.
“Ni kweli inawezekana vyanzo vya mapato vilivyopendekezwa
havitoshi kuendesha Bunge, lakini ndiyo sababu tupo hapa, haiwezekani ripoti ya
Tume iwe imekamilika pande zote,” alisema na kuongeza:
“Wamependekeza badala ya kutegemea vyanzo vya washirika,
tumependekeza kodi ya bandari ambayo ni karibu Sh3.6 trilioni inaweza kuwa ni
kodi ya Serikali ya Muungano. Kodi hiyo pekee inatosha kuendesha wizara zote
ambazo gharama yake si zaidi ya Sh3 trilioni.”
“Kuna hoja hapa, haiwezekani kuwa fedha za bandari zote
ziwe zinachangia Muungano kwani ni fedha za Tanganyika, lakini Muungano wowote
ni lazima kukubali nchi kubwa kuchangia zaidi.”
Kafulila ambaye hata baada ya kumaliza muda wake wajumbe
walipiga kelele wakitaka aendelee, alisema kwa Serikali ya Muungano kupata
mapato hayo tu, itakuwa haina haja ya kusubiri fedha za nchi washirika na pia
itakuwa na uwezo wa kuchangia fedha kwa nchi washirika.
“Haiwezekani Watanganyika wakubali kubeba gharama kubwa ya
serikali mbili badala ya gharama ndogo za serikali tatu na hii ndiyo inawapa
hofu Wazanzibari kudhani kuna kitu kinachofichwa,” alisema. Kuhusu hoja ya
kutumia maneno ya Nyerere kupinga Muungano wa serikali tatu, alisema Mwalimu
hakuwa nabii, alitazama mambo kwa wakati ule na alikuwa akibadilika kutokana na
wakati.
Alisema mwaka 1965, Mwalimu Nyerere alifuta vyama vingi...
“Angekufa mwaka huo, tungebaki kuwa alikataa vyama vingi, lakini Nyerere huyu
mwaka 1992 alikubali vyama vingi na hiyo inaonyesha kuwa kila jambo lina wakati
wake na kwa sasa hakuna namna na kupinga serikali tatu. Hivi sasa tunapata
ugumu wa lazima kutokana na misimamo ya vyama, lakini katika jambo hili la
serikali mbili na tatu na wengi wameamua.”
Alisema suala hilo likiachwa kama lilivyo waliopo
madarakani sasa wataendelea kulifunika lakini itakuja kuwa hasara kwa nchi:
“Leo mna nafasi ya kutengeneza serikali tatu kiuhalisia zaidi kuliko baadaye,
mtakosa nafasi hii, huko baadaye haiwekani kuwa na wingi huu, leo mnaweza
kuamua serikali bora zaidi, huu ni wasia tu,” alisema huku akishangiliwa.
Akizungumzia uwiano, alisema mataifa yote duniani
yanapoungana huwa hayana uwiano ulio sawa.
Alisema Jimbo la California peke yake nchini Marekani
linachangia zaidi ya asilimia 20 ya mapato yote.
Baada ya kutoka nje ya Ukumbi wa Bunge, Kafulila ambaye
alichambua kwa kina takwimu za Tume ya Warioba (soma habari yake Uk.13) alipokewa
kwa shangwe na wajumbe wa kundi la Ukawa, wakimsifia kwa kuzungumza kishujaa

Chapisha Maoni